Plan International yazindua mradi utakaogharimu Bilioni moja
Na Jacquiline Mrisho – Ifakara
mwambawahabari
Shirika la Plan International limezindua mradi wa miaka minne wa kuzuia ndoa za utotoni utakaogharimu jumla ya shilingi bilioni moja ukiwa na lengo la kumuinua mtoto wa kike kijinsia, kiuchumi na kijamii.
Mradi huo umezinduliwa rasmi na Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani yaliyoandaliwa na shirika hilo na kufanyika katika Kijiji cha Ihenga kilichopo wilayani humo.
Ihunyo amesema kuwa ndoa za utotoni ni changamoto moja wapo inayowakabili watoto wa kike na kuwafanya wasifikie malengo waliyojipangia hivyo, ametoa rai kwa Serikali na mashirika mbalimbali kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha tatizo hilo linakomeshwa.
“Ndugu wananchi, kwa kutambua changamoto zinazowakabili wasichana wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Shirika la Plan International limeandaa mradi maalum kwa ajili yao ambao utatekelezwa katika Kata nne za Idete, Mofu, Namwawala na Kisawasawa ambapo vijiji 13 vitafikiwa na mradi huo”, alisema Ihunyo.
Mkuu wa Wilaya huyo amelishukuru shirika hilo kwa mchango wao katika kuhakikisha wasichana wanapata haki zao za kukua na kuendelezwa kama watu wengine kwa kuwajengea uwezo kielimu na kimtazamo utakaowasaidia kujitambua na kupinga ndoa hizo.
Kwa upande wake Meneja wa Shirika hilo (Ifakara), Majani Rwambali amesema kuwa Shirika limeamua kuanzisha mradi huo katika Mkoa wa Morogoro kwa sababu ni mkoa mmoja wapo kati ya mikoa iliyoathirika na tatizo hilo hivyo, wanashirikiana na Serikali kuzuia ndoa hizo zinazosababisha wasichana kushindwa kufikia malengo yao.
“Asilimia 42 ya watu wanaoolewa katika Mkoa huu wapo chini ya umri wa miaka 18, hii inaonyesha dhahiri tatizo hili ni kubwa mkoani hapa kwahiyo, mradi huu unalenga kuwawezesha wasichana kujitambua na kuweza kusema hapana pamoja na kuwa na uelewa wa kutoa taarifa mapema pindi waonapo hali hiyo, hii itasaidia kukomesha tatizo hili”, alisema Rwambali.
Amefafanua njia zitakazotumika katika kuhakikisha wasichana wanapata elimu hiyo zikiwemo za kufungua klabu katika shule mbalimbali ili kuwapa mafunzo juu ya athari ya ndoa za utotoni, kushirikiana na Serikali katika kufanya vikao vya hadhara ili kuwaelimisha wananchi pia kuandaa mabonanza ya michezo kwa ajili ya kufikisha ujumbe wa kupambana na ndoa za utotoni.
Post a Comment