NBC waipongeza Plan International kwa mchango wao katika kusimamia maendeleo ya vijana
Na Jacquiline Mrisho
mwambawahabari
Benki ya NBC imelipongeza Shirika la Plan International kwa mchango wao katika kusimamia maendeleo ya vijana waliopo chini ya Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi – Dar es Salaam (DYEE) wenye lengo la kuwakwamua vijana kutoka katika lindi la umasikini.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mikopo cha Benki ya NBC, Isidory Msacky wakati wa mahafali ya mwisho ya vijana waliopo chini ya mradi huo waliohitimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi cha Future World.
Msacky amesema kuwa Shirika hilo linafanya kazi kubwa katika kusimamia miradi mbalimbali ya kuwasaidia wananchi hasa katika kuhakikisha vijana wanapatiwa elimu bora ya ufundi ambayo ni nguzo muhimu ya kuwainua na kuondokana na hali duni za maisha wanayoishi.
“Plan International ni moja kati ya mashirika ambayo tunajivunia kufanya nayo kazi katika kuisaidia jamii kwani tunatambua mchango wao katika kusimamia mafunzo ya vijana na ufuatiliaji wa maendeleo yao baada ya kuhitimu mafunzo hayo”, alisema Msacky.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi cha Future World, Robert Mkolla amesema kuwa ukosefu wa ajira kwa vijana ambao ndio asilimia kubwa ya watanzania ni janga kubwa kiuchumi na kiusalama kwani vitendo vingi viovu vinafanywa na vijana wasio na kazi za kuwaingizia vipato.
“Napenda kuzipongeza juhudi za wadau mbalimbali walioshiriki katika mradi huu wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi – Dar es Salaam (DYEE) kuanzia hatua za awali hadi leo unapofikia tamati, nawashukuru sana Benki ya NBC pamoja na Shirika la Plan International ambao ndio waliokuwa wadau mama wa mradi huu”, alisema Mkolla.
Naye Muwakilishi wa Mkurugenzi wa Plan International – Tanzania, Bi. Gwynneth Wong amesema kuwa mradi huu umeokoa vijana kutoka katika mazingira hatarishi na kuwafanya wawe na uwezo wa kujitegemea kwa kujishughulisha na biashara mbalimbali za halali.
Ameongeza kuwa asilimia 65 ya vijana 1225 waliohitimu mafunzo hayo wameajiriwa na wengine wamejiajiri hivyo inaonyesha dhahiri kuwa miradi hii ya kuwainua vijana kiuchumi inaleta mafanikio makubwa kwa vijana na taifa kiujumla.
Mradi huu wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi - Dar es Salaam (DYEE) kupitia mafunzo ya stadi za kujiajiri (BEST Model) umefadhiliwa na Benki ya NBC na kuratibiwa na Shirika la Plan International, umetekelezwa katika kipindi cha miaka 3 na umetoa mafunzo kwa jumla ya vijana 1,225.
Post a Comment