Vijana nchini washauriwa kujiajiri kupitia Sanaa.
Na Shamimu Nyaki- WHUSM.
mwambawahabari
Katika kukabiliana na upungufu wa ajira hapa nchini Vijana wameshauriwa kujiajiri kupitia Sanaa na vipaji walivonavyo katika kupata kipato.
Ushauri huo umetolewa jana Wilayani Bagamoyo na Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bibi Leah Kihimbi alipokuwa anawahutubia wahitimu wa Astashahada na Stashahada ya Sanaa na Ufundi katika Chuo cha Sanaa na Ufundi Bagamoyo kilichopo chini ya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa).
“Tumieni elimu mliyopata kujiajiri wenyewe ili kuepuka changamoto ya ajira iliyopo hapa nchini, ujuzi mliopata ni njia pekee ya kujiletea kipato na Taifa kwa ujumla”.Alisema Bibi Leah.
Aidha Kaimu Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa wasanii wote wanaofanya kazi za Sanaa ni vyema wakasajili kazi zao katika Mamlaka husika ili iwe rahisi kwa Serikali kutoa msaada kwa urahisi kwaWasanii hao.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu waTaasisi ya Sanaa na Utmaduni Bagamoyo (TaSUBa) Dkt.Herbet Makoye aliwasihi wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri wa sanaa watakapokuwa wanafanya shughuli zao za Sanaa.
“Nendeni mkawe mabalozi wazuri wa Chuo chetu kwa kuwa Wasanii bora na kutengeneza kazi nzuri ili muweze kushindana na soko la ajira”. Alisisitiza Dkt.Makoye.
Naye mhitimu wa ngazi ya Stashahada ya Sanaa na Ufundi Bi Imelda John amesema kuwa elimu aliyoipata itamsaidia kufanya kazi ya Sanaa kwa weledi zaidi hasa katika fani ya kutengeneza Filamu na Picha Jongefu.
Mahafali hayo ni ya 27 katika chuo hicho ambapo kwa mwaka huu jumla ya wanafunzi 85 wametimu Astashahada na Stashahada ya Sanaa na Ufundi.

Post a Comment