Ads

MSEMAJI WA SERIKALI: WAZIRI HATOKUWA NA MAMLAKA MAKUBWA KATIKA MUSWADA WA HABARI


Na Beatrice Lyimo 
mwambawahabari
SERIKALI imesema hakutokuwa na matumizi mabaya ya mamlaka anayopewa Waziri anayesimamia tasnia ya habari katika muswada wa sheria ya huduma ya habari isipokuwa kwa masuala yatakayohatarisha usalama wa Taifa.

Imesema Serikali haiwazuii waandishi wa habari kukosoa sera, matamko na ahadi mbalimbali zinazotolewa na Viongozi wa kitaifa pindi wanaposhindwa kutekeleza maagizo wanayoyatoa kwa wananchi.

Akizungumza katika mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea vyombo mbalimbali vya habari leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO), Hassan Abbas alisema muswada huo unatoa fursa kwa chombo cha habari kupeleka malalamiko yake mahakamani pindi inapotokea kutokubaliana na hatua itakayoweza kuchuliwa na  Waziri mwenye dhamana ya habari.


 Kwa mujibu wa Abbasi alisema yapo masuala kadhaa yanayopaswa kuchuliwa hatua za haraka za maamuzi ikiwemo suala la uchochezi, uasi wa kikundi fulani cha watu kinachotaka kuigombanisha Serikali na wananchi.

Aliongeza kuwa hata katika mikataba ya kimataifa ikiwemo kifungu cha 19 mkataba wa geneva wa mwaka 1966 umeeleza kuhusu haki ya kupata habari na taarifa ingawa upo ukomo katika masuala kadhaa ikiwemo suala la usalama wa taifa.

“Uchochezi ni kuhatarisha amani ya nchi, lakini mwandishi  akiikosoa Serikali haitokuwa uchochezi bali kwa atakayeleta habari za uchochezi kwa maana ya uasi atatakiwa kuwajibishwa” alifafanua Mkurugenzi Abbas.

Aidha alisema kuwa muswada huo umekusudia kuanzishwa kwa Baraza la Maadili litakalokuwa na wajumbe saba, ambapo wanne kati yao ni kutoka katika tasnia ya habari ikiwemo mwenyekiti wa Baraza na watakuwa na mamlaka ya kusimamia maslahi na usalama wa waandishi.

Akifafanua zaidi alisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa mchakato wa kupata Sheria ya huduma ya habari unafika mwisho ambapo mchakato wake umechukua miaka 20 mpaka sasa.

Alisema kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa muswada huo unapitishwa na Bunge ili uweze kuwa sheria kamili na hatimaye kuifanya tansia ya habari kuwa taaluma yenye kuheshimika zaidi.

Pia alisema kuwa muswada huo utasaidia sekta ya habari kuwa muhimili wenye nguvu na taaluma iliyokamilika yenye haki zake kama upatikaji wa bima za afya kwa waandishi wa habari.

Abbasi alisema iwapo sheria hiyo itapitishwa itatumika upande wa Tanzania Bara pekee na si Zanzibar, kwa kuwa suala la habari halipo katika mambo ya Muungano, ingawa sekta hizo zinashirikiana kwa namna moja au nyingine.

No comments