Ads

MEYA ILALA: NYERERE ALIKUWA NI ZAWADI TOKA KWA MWENYEZI MUNGU



Mwambawahabari
 Na:John Luhende
IKIWA imebakia siku moja kuazimisha siku ya kumbukumbu ya kifo cha Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julias Kambarage Nyerere aliyefariki Oktoba 14 miaka 17 iliyopita, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Charles Kuyeko  amesema kiongozi huyo ambaye alikuwa Rais wa awamu ya kwanza wa Tanzania na mwasisi wa taifa la Tanzania alikuwa ni zawadi kwa watanzania toka kwa Mwenyezi Mungu na ndiyo maana pengo la kiongozi huyo halizibiki.

Mstahiki Meya ameyasema hayo katika  mahojiano na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Jijini Dar es Salaam.

Kuyeko ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Bonyokwa (Chadema) amesema kuwa, Mwalimu Nyerere anafaa kuenziwa kwa heshima na kwa vitendo kwa kuwa ni mfano mzuri wa kuigwa na watanzania na viongozi wote wa sasa, Afrika na Duniani kote.

Katika mazungumzo yake Kuyeko pia amemuelezea Mwalimu Nyerere  kuwa alikuwa ni mpenda watu, Amani, Maendeleo na mwenye maamuzi yasiyosukumwa na ushabiki wa itikadi.

Mhe.Kuyeko alisema, Mwalimu Nyerere wakati wa uongozi wake aliweka kipaumbele cha kwanza na misingi imara na bora kwenye sekta ya elimu. Ili kuhakikisha kwamba watanzania wote tunapata elimu Mwalimu aliweka misingi imara ya elimu kugharamiwa na serikali. Elimu ilitolewa bure bila ubaguzi ambapo kulikuwa hakuna utofauti kati ya tajiri na maskini tofauti na sasa elimu bure lakini bado kuna changamoto nyingi. Tulipata mahitaji yote ya shule bure si kwa kuwa kulikuwa na uchumi mkubwa, Bali  alitekeleza na kusimamia misingi yake na hakukuwa ufisadi mkubwa kama sasa.


Ameeleza kuwa, kiongozi huyo alizingatia mahitaji ya wananchi wake hususani masuala ya ajira ambapo alijenga viwanda vingi na kutoa fursa za ajira kwa vijana Tanzania tofauti na sasa ambapo viongozi wengi wanaongea bila utekelezaji.

" Enzi za utawala wa Baba wa Taifa vijana tulipewa kipaumbele, hakukuwa na uhaba wa ajira kama ilivyo sasa, yaani tulikuwa tukisoma huku tunauhakika wa ajira baada  ya kuhitimu.
Aidha, vijana tulifundishwa kuwa wazalendo na kupigania Taifa letu na ndiyo swala la usalama lilikuwa ni jukumu la watanzania wote.

Mbali na hilo, Kuyeko pia amemuelezea kiongozi huyo kuwa, alikuwa  akipata maoni ya kila mtu na kuonyesha Upendo kwa wananchi hata kupelekea wananchi kuwa wazalendo tofauti na viongozi wa sasa.

"Nyerere ilikuwa ni zawadi kutoka kwa mungu kiasi kwamba mazuri yake aliyoyafanya viongozi wengi hawatayafikia.Yeye alikua ni nuru ya Afrika ambayo iliwasaidia nchi nyingi kupata Uhuru wao". Nuru hiyo ilizimika bila kuwa na mbadala sahihi wa Viongozi wenye kipawa kama chake.

Mwalimu Nyerere alifanya mambo mengine mazuri ambayo hata nikielezea hayawezi kuisha leo,niwaombe tu viongozi mwenzangu na taifa kwa ujumla tuendelee kumuenzi kwa kufuata nyao zake huku tukiwatumikia wananchi kwa uzalendo kama alivyokuwa akifanya.

Aidha Mhe. Kuyeko amewatakia watanzania wote maazimisho mema ya siku ya kumbukumbu ya hayati Baba wa taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere.

No comments