KAMATI YA BUNGE YAENDELEA KUUJADILI MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI.
Na Mwandishi Wetu Dodoma
Mwambawahabari
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeendelea na kikao cha kujadili Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kwa kupitia kifungu kwa kifungu kwa ajili ya kuboresha Muswada huo.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba alisema kuwa baada ya kuwapa wadau muda wa wiki moja kuwasilisha maoni yao juu ya Muswada, wao kama kamati wanaendelea na majukumu yao ya kutunga sheria.
“Sisi kama Kamati tunaendelea na majukumu yetu ya kutunga hii sheria na tumeanza kupitia kifungu kwa kifungu ili kuangali namna bora ya kuuboresha muswaada huu.’’ alisistiza Mhe. Serukamba.
Mhe. Serukamba ameongeza kuwa majadiliano yao sio mwisho wa kutungwa kwa sheria hiyo bali baada ya hapo watakutana na wadau wa habari au kupitia maoni ya watu mbalimbali yaliyowasilishwa kwa njia ya maandishi ili kuiboresha zaidi sheria hii.
Kwa upande wake Mbunge wa Kakonko Mhe. Kasuku Bilago alisema kuwa Muswada huo bado unahitaji kufanyiwa marekebisho na wao kama wajumbe wa Kamati wanaendelea kuupitia Muswaada huo kwa makini kwa kuuchambua kila kipengele na hatimaye kupata Sheria iliyo bora.
“Hatutungi Sheria kwa manufaa ya Serikali sisi wabunge tunatunga Sheria kwa ajili ya wananchi kwahiyo tuzingatie sana maoni ya wadau ili kupata Sheria itakayoleta madadiliko katika Tasnia ya Habari nchini” alisema Mhe. Bilago.
Naye Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Ruvuma Mhe. Sikudhani Chikambo alisema muswada huo ni tofauti na miswada iliyoletwa kipindi cha nyuma kwani umeboreshwa na kwa kiasi kikubwa umezingatia maoni ya wadau wa habari ambao ndio wahusika wakuu wa muswada huu.
“ Muswada huu utawaweka waandishi wa habari katika sehemu nzuri za kujua ukomo wa majukumu yao na kuzingatia weledi na kufuata taratibu na sheria katika kutekeleza majukumu yao alisema,”” alisema Mhe. Sikudhani.
Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii inaendelea na majukumu yake ya kujadili, kuchambua na kuboresha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 kesho kabla ya hatua nyingine.
Post a Comment