Ads

Serikali kukamilisha Miradi ya Maji



Na Raymond Mushumbusi 
mwambawahabariblog
 
Serikali kushirikiana na Benki ya Dunia imejipanga kukamilisha Miradi ya Maji iliyopo katika maeneo tofauti nchini ili kuondoa shida ya upatikanaji wa maji safi na salama  katika Vijiji,Miji,Wilaya na Mikoa.
 
Akijibu swali la Mhe.Flatei Gregory Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini (CCM) lililouliza, Serikali imejipangaje kumaliza miradi hii ili wananchi wapate maji hasa wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini ,Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwela amesema miradi ya maji mbalimbali ipo katika hatua za utekelezaji wake ili kuikamilisha ndani ya muda uliopangwa na kuwezesha maji safi na salama kupatikana kwa wananchi.
 
“ Tuna jumla ya miradi takribani 1853 na miradi 1143 tayari imekamilika na miradi 434 ipo karibu kukamilika ili kuanza kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi walipo karibu na mradi huo”
 
“ Napenda kumueleza Mhe. Mbunge kuwa miradi ya maji ya Haydom, Masienda, Tumati, Arri na Bwawa la Dongobesh ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake na miradi yote hiyo imemalizika kwa asilimia 45 mpaka sasa na miradi hii ya maji niliyoitaja ikikamilika itaweza kuhudumia wananchi kama ifuatavyo Mradi wa Maji wa Haydom utakapokamilika utahudumia wakazi wapatao 16,737, Mradi wa Maji wa Masieda utahudumia wakazi 3,137, Mradi wa Arri utahudumia wakazi 17,580” Alisema Mhe. Kamwela.
 
Akijibu swali la nyongeza toka kwa Mhe.Flatei Gregory Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini (CCM)  lililouliza kwanini miradi hii inachelewa kukamilika, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhe. Isack Kamwela amesema miradi hii inachelewa kukamilika kutokana na upatikanaji wa fedha za kuwalipa wakandarasi kutopatikana kwa wakati ila Serikali inaendelea kutafuta fedha kila zinapopatikana ili kukamilisha miradi hiyo.
 

Serikali kupitia Wizara wa Maji na Umwagiliaji imejipanga kuanzisha na kuendeleza miradi mingi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini ili kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi.

No comments