Na lilian Lundo
mwambawahabariblog
Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa leo amezindua mwongozo wa utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa sera ya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika mkutano wa wadau wa uwezeshaji kiuchumi.
Mkutano huo ambao umeandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji (NEEC) umeshirikisha wadau mbalimbali kama vile Tanzania Investment Bank(TIB), Tanzania Poster Bank (TPB), UTT Microfinance, World Vision, CRDB, National Housing Cooperation (NHC), PSPF, GEPF ambao wanachangia katika kuendeleza uchumi wa mwananchi.
Katika hotuba yake Mhe. Majaliwa alisema kuwa utekelezaji wa kila siku wa Serikali unamlenga mwananchi wa hali ya chini ili kumuinua kiuchumi. Hivyo amewataka wadau wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kusaidiana na Serikali katika kuinua uchumi wa mwananchi wa hali ya chini.
“Katika kikao hiki angalieni maeneo ambayo yanalenga matokeo ya haraka kama vile kilimo, uvuvi, viwanda, ufugaji, biashara, utalii na madini ili kumwezesha mwananchi wa chini kujikwamua kimaisha na kuinua uchumi wake,” alisema Mhe. Majaliwa.
Aidha,Mhe. Majaliwa aliwataka wadau wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kushirikisha wananchi katika kujenga uchumi na kuwasaidia kupata mitaji kwa gharama nafuu ambayo itazingatia riba itakayokuwa rahisi kwa mwananchi wa kawaida kuweza kuirudisha kutokana na biashara anayoifanya.
Mhe. Majaliwa ameitaka NEEC kuangalia namna gani mtaala wa ujasiriamali utaanza kufundishwa kuanzia elimu ya msingi mpaka vyuo vikuu ili kuondokana na tatizo la ajira kwa vijana ilikuwawezesha kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa na Serikali au mashirika binafsi.
Dira ya Maendeleo ya Taifa imeainisha kuwa ifikapo mwaka 2025 sehemu kubwa ya uchumi wa Tanzania iwe inamilikiwa na Watanzania wenyewe, hivyo shughuli zote za uwezeshaji zinatakiwa zifanywe kwa ushiriki wa wadau wote ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufanyia biashara na fursa sawa za biashara ndani na nje ya nchi.
Post a Comment