Na Beatice Lyimo
mwambawahabariblog
Shirikisho la wamiliki
wa shule na vyuo visivyo vya serikali TAMONGSO watoa pongezi kwa
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi Teknolojia na Ufundi kwa kuliagiza
Baraza la Taifa la Mitihani kufuta mfumo unaotumika sasa wa Wastani wa Alama
(GPA) na kurudi katika mfumo uliokuwa unatumika hapo awali wa division.
Akizungumza na waandishi
wa habari leo jijini Dar es salaam Mwenyekiti Taifa wa TAMONGSO Bwa. Mrinde
Mzava amesema kuwa Waziri wa Elimu Ameitendea haki Sekta ya Elimu kwani mfumo
huo ulileta sintofahamu kwa wananchi wengi.
“Waziri ameitendea haki
sekta ya Elimu kwani mfumo wa GPA ulileta sintofahamu kwa wananchi na pia
ulikuwa unaongeza ufaulu usio na mashiko kwa wanafunzi walio wengi
ukilinganisha na mfumo uliokuwa unatumika awali,” aliongeza Mwenyekiti huyo.
Vilevile Mwenyekiti huyo
alisema kuwa Tanzania inahitaji kuingia kwenye soko la upinzani hasa katika
sekta ya Elimu ili iweze kuajiri watu wenye utaalamu na sifa stahiki
na kuweza kushindanishwa kwenye soko la kimataifa hivyo kwa mfumo wa GPA
ulikuwa unadidimiza elimu ya Tanzania.
Mbali na hayo Mwenyekiti
huyo alitoa agizo kwa baadhi wamiliki wa shule na vyuo visivyo vya Serikali
kutotumia kigezo cha pesa ili kudidimiza kiwango cha Elimu nchini.
Kwa upande wake Makamu
Mwenyekiti wa shirikisho hilo Bwa. Emmanueli Gwegenyeza ameshauri viongozi na
wananchi kwa ujumla kutochanganya suala la Siasa na Elimu kwani kwa kufanya
hivyo tutazidi kudidimiza Sekta ya Elimu nchini.
“Tusiingize suala na
Siasa na Elimu kwa wakati mmoja kwani kwa kufanya hivyo tunaweza kuididimiza
Sekta ya Elimu pia tunaahidi kumpa Waziri ushirikiano ili kuzidi kuinua Sekta
ya Elimu nchini,” aliongeza Makamu huyo.
Post a Comment