Watakaofanya fujo mkesha wa mwaka mpya kukiona
Na Jacquiline Mrisho mwambawahabari
Jeshi la Polisi Kanda
maalum ya Dar es salaam limewatahadharisha wananchi kutokufanya fujo wakati wa
mkesha wa mwaka mpya kwa kuweka mikakati mikali kwa watakaokaidi amri
hiyo.
Akizungumza na Waandishi
wa Habari leo Jijini Dar es salaam Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es
salaam Suleiman Kova amepiga marufuku uchomaji wa matairi ya gari,
upigaji baruti, risasi za moto na fataki ambazo zaweza kusababisha
madhara wakati wa mkesha wa mwaka mpya.
“ Ni baraka zaidi
kusherekea sherehe kama hizi kifamilia na sio vizuri kuingia mwaka mpya ukiwa
mahabusu, huo ni mkosi” Alisema Kamishna Kova.
Kamishna Suleiman Kova
aliongeza kuwa watashirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Jeshi la
Zimamoto, kampuni binafsi za ulinzi, vikundi vya ulinzi shirikishi pamoja na
kutumia ndege za Polisi kufanya doria ili kuhakikisha kuwa wanailinda amani na
kudhibiti aina yoyote ya uhalifu utakaojitokeza.
Aidha Kamishna Kova
amesisitiza kuwa vituo vyote vya polisi vitakuwa wazi masaa 24 ili kuwawezesha
wananchi kutoa taarifa haraka pindi wanapopata matatizo au wanapoona dalili
zozote za uvunjifu wa amani pia amehakikisha kuwa fukwe zote za bahari na
maeneo yote yenye mikusanyiko yatalindwa.
Katika kipindi hiki cha
kuelekea mwisho wa mwaka wa 2015 Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam
limetoa rai kwa wananchi kushirikiana na Jeshi hilo katika kuzuia uhalifu kwa
kutoa taarifa haraka pindi waonapo dalili za uvunjifu wa amani.
Post a Comment