Ads

URUWA WAMPONGEZA MAGUFULI

Na Lilian Lundo MAELEZO

Uongozi unaounda mashirikiano ya umoja wa vyama visivyo na Ruzuku ya Serikali ambavyo ni  ADA-TADEA, UDP, UPDP na SAU uitwao URUWA (Umoja wa Rufaa ya Wananchi) umeipongeza Serikali ya Awamu ya Tano kwa uongozi uliojaa utukufu wa uzalendo.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa URUWA John Shibuda leo Jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongeo na waandishi wa habari.

“Tunamuunga mkono Rais John Pombe Magufuli kwa juhudi zake za utumishi aminifu na tiifu kwa ustawi na maendeleo ya Jamii na Taifa, hongera sana kwa uongozi wako uliojaa utukufu wa uzalendo na Neema ya kauli aminifu ya HAPA KAZI TU ambayo ipo kwa maslahi ya Tanzania,” alisema Shibuda.

Umoja huo pia umepongeza mshikamano wa uzalendo na uwajibikaji makini unaotekelezwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu  Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa.

Shibuda aliongeza kwa kusema kuwa wananchi wa makundi yote yasiyotarajia kuingia katika kundi la uchumi wa kati sasa wanamatumaini ya kufikia uchumi wa kati kutokana na kupata utumishi sikivu kwa vilio vyao vya muda mrefu vya kupata maisha bora.

Aidha, uongozi wa umoja huo umesema kwamba unaunga mkono juhudi zote zinazotekeleza Serikali ya Awamu ya Tano katika kulisukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Jamii na Taifa. Pia wameitaka Serikali ya Awamu ya Tano kuendelea kutakatisha na kung’arisha usafi wa mazingira ya uwajibikaji wa safari ya ukombozi ya ASP na TANU.

Umoja wa vyama visivyo na Ruzuku ya Serikali URUWA umeundwa tarehe 18/12/2015  huku Mwenyekiti wa Umoja huo akiwa ni John Shibuda  ambaye ni Katibu Mkuu- ADA-TADEA, Katibu Mkuu akiwa ni Fahami Nassoro Dovutwa ambaye ni Mwenyekiti Taifa – UPDP.

Wajumbe wa umoja huo ni Isaac Cheyo ambaye  Katibu Mkuu – UDP, Paul Kyara   Mwenyekiti SAU na Yusufu Manyanga  ni Makamu Mwenyekiti – SAU.
Viambatisho 3

No comments