Ads

WAZIRI WA NISHATI AIPONGEZA PURA KWA KUVUKA MALENGO, AITAKA KUIMARISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI NA RASILIMALI ZA NDANI

 


DAR ES SALAAM, Novemba 26, 2026 Waziri wa Nishati, Dkt.Juma Homela, amelipongeza Baraza la Wafanyakazi la Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kwa utendaji kazi uliowezesha mamlaka hiyo kuvuka malengo yake kwa asilimia 100, huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano, ushirikiano na uzingatiaji wa sheria na kanuni katika utekelezaji wa majukumu yao.


Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa PURA jijini Dar es Salaam, Waziri Homela alisema ushirikiano kati ya waajiri na wafanyakazi ni msingi muhimu wa kuongeza ufanisi katika taasisi za umma na kuchochea maendeleo ya sekta ya nishati.


Alieleza kuwa misingi ya ushirikiano huo imeainishwa katika sheria mbalimbali, zikiwemo Sheria ya Utumishi wa Umma, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini pamoja na Sheria ya Taasisi za Kazi, ambazo zinalenga kuimarisha mahusiano mazuri kazini na kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu.


Katika kikao hicho, Waziri Homela alitoa maelekezo na kusisitiza vipaumbele kadhaa vya Serikali vinavyopaswa kupewa uzito katika utekelezaji wa majukumu ya PURA.


Kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia, aliitaka PURA kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama, hususan gesi asilia, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Alisisitiza pia umuhimu wa kuchangia juhudi za kupunguza uzalishaji wa gesi chafuzi kuelekea mwaka 2050.


Aidha, aliitaka PURA kutambua na kutumia fursa za kiuchumi zinazotokana na soko la hewa ukaa (Carbon Market), pamoja na kuimarisha matumizi ya teknolojia ya ukamataji, utumiaji na uhifadhi wa hewa ukaa (CCUS). Alibainisha umuhimu wa kushirikiana na wadau wa kimataifa kupitia programu mbalimbali, ikiwemo *Energy for Development (EfD)*, ili kuongeza ujuzi na kuvutia uwekezaji katika eneo hilo.


Katika hatua nyingine, Waziri Homela aliielekeza PURA kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuhakikisha zinatolewa leseni nne za utafiti wa mafuta na gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo maeneo ya kaskazini mwa Tanzania. Hatua hiyo inalenga kuongeza wigo wa utafiti na kuchochea ugunduzi wa rasilimali za mafuta na gesi asilia nchini.


Kuhusu maendeleo ya wataalamu wa ndani, alisisitiza umuhimu wa kuwapa kipaumbele Watanzania katika kujengewa uwezo kupitia mafunzo, uhamishaji wa teknolojia na matumizi ya rasilimali zilizopo. Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha kuwa sekta ya nishati inawanufaisha wananchi na kuongeza ushiriki wa wataalamu wa ndani katika shughuli za sekta hiyo.


Akihitimisha hotuba yake, Waziri Homela aliwataka viongozi na wafanyakazi wa PURA kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii, weledi, uadilifu na uzalendo, akisisitiza kuwa mshikamano na uwajibikaji ni nguzo muhimu katika kukuza sekta ya nishati na kuchangia maendeleo ya taifa.


No comments