COSTECH YASHEREHEKEA MIAKA 40 YA MAFANIKIO, YAKIJIWEKA TAYARI KUTEKELEZA DIRA YA TAIFA YA MAENDELEO 2050
Mwamba wa habari
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Muhunda Nungu, amesema maadhimisho ya miaka 40 ya COSTECH ni fursa muhimu ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana, hali ya sasa na mwelekeo wa taasisi hiyo katika kuchochea maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Nungu amesema COSTECH inajivunia kuendelea kuwepo na kutekeleza majukumu yake kwa miaka 40, ikiwa ni ishara ya umuhimu wa taasisi hiyo katika kuendeleza tafiti, teknolojia na ubunifu kwa manufaa ya Taifa.
Amesema mafanikio ya COSTECH yana mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inategemea sayansi, teknolojia na ubunifu katika kuboresha maisha ya Watanzania, kuongeza tija katika uzalishaji, hususan sekta za afya na kilimo, pamoja na kukuza uchumi.
Aidha, ameeleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika kukuza utamaduni wa ubunifu, ambapo vijana na watafiti wameendelea kubuni suluhisho mbalimbali, zikiwemo bidhaa na huduma ambazo tayari zimeingia sokoni.
Katika kuadhimisha miaka 40, COSTECH imeandaa mijadala inayolenga kuangalia mustakabali wa sayansi na teknolojia nchini, vipaumbele vya utafiti, ushirikiano wa kimataifa na nafasi ya sekta binafsi katika kukuza ubunifu.
Amebainisha pia kuwa COSTECH inaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi na uchakataji wa taarifa za utafiti na ubunifu kupitia mfumo wa NIST, ambao unatarajiwa kutoa taarifa na ripoti zitakazosaidia kufanya maamuzi na kupanga vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.
Katika kuimarisha mazingira ya ubunifu, Dkt. Nungu amesema COSTECH inaendelea kupanua huduma za kuwawezesha wabunifu kupitia vituo kama Buni Hub na Tanzania Development and Innovation Business Incubator (DTBi), pamoja na mipango ya kupanua wigo wa huduma hizo hadi Dodoma.
Amesisitiza kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa katika kufanikisha Dira ya 2050, hivyo ni muhimu kuwawezesha vijana wabunifu kuanzisha kampuni, kukuza biashara zao na kuendeleza suluhisho zinazoweza kutatua changamoto za jamii.
"Mafanikio tuliyoyapata katika miaka 40 yanatupa sababu ya kujivunia, lakini bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha sayansi, teknolojia na ubunifu vinakuwa chachu ya maendeleo ya Taifa."

Post a Comment