TISEZA YASAJILI MIRADI 3,538 YENYE THAMANI YA DOLA BILIONI 68.6
Miradi 3,538 ya uwekezaji yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 68.6, sawa na takribani shilingi trilioni 150, imesajiliwa nchini katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026, huku ikitarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya milioni moja.
Akizungumza katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari uliojadili utendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) katika kipindi cha miaka sita, Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Gilead Teri, amesema sekta ya viwanda imeongoza kwa kusajili miradi 1,061, ikifuatiwa na sekta ya uchukuzi yenye miradi 525.
Amesema sekta nyingine zilizochangia idadi hiyo ni utalii yenye miradi 335, kilimo miradi 308 na majengo ya kibiashara miradi 301.
Kuhusu umiliki, Teri amesema miradi 1,619 inamilikiwa na wawekezaji wa kigeni, miradi 1,158 inamilikiwa na Watanzania, huku miradi 361 ikiwa ya ubia kati ya wawekezaji wa ndani na wa nje.
Ameeleza kuwa China inaongoza kwa kuchangia mitaji mikubwa ya uwekezaji yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 14.1, ikifuatiwa na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wenye bilioni 5.039, Mauritius bilioni 2.1, Uingereza bilioni 1.6 na India bilioni 1.5.
Akizungumzia mipango ya mwaka 2027, amesema TISEZA inalenga kuwawezesha wazalishaji wadogo kupata masoko ya kimataifa, kuendeleza maeneo maalum ya kiuchumi na kuimarisha mifumo ya usajili wa biashara na maeneo huru ya kiuchumi.

Post a Comment