Ads

TAMASHA LA MZIZIMA KUADHIMISHA NA KUENDELEZA MILA, DESTURI NA UTAMADUNI WA MTANZANIA







Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Taasisi ya Pamoja Tutashinda Tanzania (PATUTA), Dkt. Aidan Ndaombwa, ametangaza maandalizi ya Tamasha la Mzizima, linalolenga kuadhimisha, kuhifadhi na kuendeleza mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania, sambamba na kuenzi historia ya Jiji la Dar es Salaam, ambalo zamani lilijulikana kwa jina la Mzizima.

Akizungumza kuhusu tamasha hilo, Dkt. Ndaombwa amesema kuwa tamasha hilo litafanyika kwa siku tatu, kuanzia Desemba 11 hadi 13 katika Viwanja vya Kimataifa, likiwa na lengo la kuwakutanisha Watanzania kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kujifunza, kuonesha na kuthamini urithi wao wa kitamaduni.

Amesema tamasha hilo litashirikisha vikundi vya ngoma za asili kutoka mikoa isiyopungua 26, hatua inayolenga kuonesha utajiri wa tamaduni za makabila mbalimbali nchini na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Aidha, amesema kuwa tamasha hilo litakuwa na shughuli mbalimbali za kiutamaduni na kihistoria, ikiwemo michezo ya asili kama bao, ambayo ni sehemu ya urithi wa jamii za Kitanzania.

Katika eneo la historia, tamasha hilo litaangazia maendeleo ya usafiri jijini Dar es Salaam, ikiwemo historia ya usafiri wa UDA na magari ya Daradara, ili kuwapa wananchi, hususan vijana, fursa ya kufahamu mabadiliko ya mifumo ya usafiri katika nyakati tofauti.

Vilevile, kutakuwa na maonesho yanayohusisha historia ya waasisi wa taifa, yakiwemo maudhui yanayohusu baiskeli ya Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wake katika historia ya Tanzania.

Dkt. Ndaombwa ameeleza kuwa tamasha hilo pia litatoa nafasi ya mijadala kuhusu maadili ya vijana, kwa lengo la kujenga uelewa juu ya umuhimu wa maadili mema, uzalendo na uwajibikaji katika jamii.

Amesisitiza kuwa Tamasha la Mzizima si tukio la burudani pekee, bali ni jukwaa la kuelimisha jamii, kuhifadhi historia na kuhakikisha kuwa mila, desturi na utamaduni wa Mtanzania vinaendelea kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Tamasha hilo linatarajiwa kuwa fursa muhimu ya kuenzi utambulisho wa Mtanzania na kuikumbusha jamii historia ya Dar es Salaam, kuanzia enzi za Mzizima hadi maendeleo yake ya sasa.




No comments