Ads

TANAPA YATAJA MAFANIKIO MAKUBWA YA UHIFADHI KATIKA MIAKA MITANO YA SERIKALI YA AWAMU YA SITA

  


Na.Hashim Mushi

Dar es salaam.

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limetangaza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta ya uhifadhi, ikolojia na utalii nchini katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.


Mafanikio hayo yameelezwa na Kamishna wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Missana Mwishawa, alipokuwa akizungumza katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari, ambapo alieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na shirika hilo kuimarisha uhifadhi na kukuza utalii nchini.


Amesema katika kipindi hicho, TANAPA imefanikiwa kuimarisha ulinzi na usalama katika hifadhi za taifa kwa kutekeleza jumla ya doria 301,314, ambazo ni sawa na zaidi ya asilimia 98 ya mpango kazi uliokuwa umepangwa.


Alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwepo wa vifaa na zana za kisasa za kazi, mafunzo kwa watumishi, nidhamu, ari ya kazi pamoja na upatikanaji wa fedha zilizowezesha kutekelezwa kwa shughuli za uhifadhi.


Kupitia doria hizo, jumla ya watuhumiwa 30,559 wanaohusishwa na vitendo vya ujangili, uingizaji haramu wa mifugo na ukataji miti wamekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa hatua zaidi.


Katika hatua nyingine, Kamishna huyo alieleza kuwa TANAPA imeendelea kuchukua hatua za kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyama pori, ambayo imekuwa ikiongezeka kutokana na mabadiliko ya matumizi ya ardhi na ongezeko la idadi ya watu.


Amesema shirika hilo limekuwa likitumia teknolojia za kisasa, zikiwemo ndege zisizo na rubani (drones) na mikanda maalumu yenye mfumo wa GPS inayofungwa kwa baadhi ya wanyama ili kufuatilia mienendo yao na kuchukua hatua za kuwazuia wanapokaribia maeneo ya makazi ya wananchi.


Alibainisha kuwa matumizi ya teknolojia hizo yanalenga kuimarisha ulinzi wa wananchi na mali zao, huku yakihakikisha wanyama pori wanabaki katika maeneo yao ya asili.


Kuhusu kukuza uchumi wa wananchi wanaozunguka hifadhi, Kamishna huyo amesisitiza umuhimu wa wadau wa utalii, hususan wamiliki wa hoteli na kampuni za utalii, kutumia na kununua bidhaa zinazozalishwa nchini.


Amesema hatua hiyo itasaidia kuwapatia wakulima, wafugaji na viwanda vya ndani soko la uhakika, kuongeza ajira na kukuza kipato cha wananchi, sambamba na kuimarisha mnyororo wa thamani katika sekta ya utalii.


Aidha, amesisitiza kuwa TANAPA itaendelea kushirikiana na serikali za mitaa, jamii zinazozunguka hifadhi pamoja na wizara na taasisi mbalimbali za serikali kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinaendelea kuwa endelevu na kuleta manufaa kwa taifa.


Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho, huku sekta ya utalii ikiendelea kuchangia ukuaji wa uchumi na pato la taifa.


No comments