Ads

IIA TANZANIA NA DSE WASAINI HATI YA MAKUBALIANO KUIMARISHA UTAWALA BORA

 


NA KAROLI VISENT

TAASISI ya Wakaguzi wa Ndani Tanzania (IIA Tanzania) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) zimesaini Hati ya Makubaliano (MoU) kwa lengo la kuimarisha mafunzo ya kitaaluma, tafiti kuhusu Kielezo cha Utawala Bora wa Kampuni (Corporate Governance Index), pamoja na uandaaji na uchapishaji wa machapisho ya kitaaluma.


Ushirikiano huo unalenga kuunganisha utaalamu na uzoefu wa taasisi hizo mbili katika kuhamasisha uelewa na utekelezaji wa misingi bora ya utawala bora katika kampuni na taasisi mbalimbali nchini.


Kupitia makubaliano hayo, taasisi hizo zitashirikiana kuimarisha uwajibikaji, uwazi, usimamizi wa vihatarishi pamoja na ufanisi wa mifumo ya udhibiti wa ndani.


Katika eneo la mafunzo na maendeleo ya kitaaluma, ushirikiano huo utalenga kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi, wajumbe wa kamati za ukaguzi, watendaji wakuu, wakaguzi wa ndani pamoja na wataalamu wanaohusika na usimamizi wa vihatarishi, uzingatiaji wa sheria na kanuni na utawala bora.


Mafunzo hayo yatahusisha maeneo mbalimbali ikiwemo majukumu ya bodi na menejimenti, usimamizi wa vihatarishi, mifumo ya udhibiti wa ndani, maadili ya kitaaluma, uwazi katika utoaji wa taarifa na mchango wa ukaguzi wa ndani katika kuimarisha usimamizi wa taasisi.


Aidha, IIA Tanzania na DSE zitashirikiana kufanya tafiti kuhusu Kielezo cha Utawala Bora wa Kampuni, ambacho kinatarajiwa kutoa taswira ya hali ya utawala bora nchini, kubaini mafanikio yaliyofikiwa na changamoto zinazohitaji maboresho.


Tafiti hizo pia zitachunguza ufanisi wa bodi na kamati za ukaguzi, uwajibikaji wa menejimenti, usimamizi wa vihatarishi, mifumo ya udhibiti wa ndani na utekelezaji wa maadili, pamoja na namna taasisi zinavyolinda maslahi ya wanahisa na wadau wengine.


Matokeo ya tafiti hizo yanatarajiwa kutoa mapendekezo yanayotokana na ushahidi yatakayosaidia kampuni na taasisi kuboresha mifumo yao ya utawala na utendaji kazi, huku yakichangia mijadala ya kitaaluma kuhusu uwajibikaji na uwazi katika mazingira ya biashara na uwekezaji.


Vilevile, makubaliano hayo yanajumuisha maandalizi na uchapishaji wa ripoti za kitaaluma na machapisho yatakayosaidia kusambaza maarifa yatakayozalishwa kupitia tafiti na uzoefu wa kitaaluma.


Ushirikiano huo unatarajiwa kuchangia kuimarisha utawala bora nchini kwa kuunganisha utaalamu wa ukaguzi wa ndani na uzoefu katika masoko ya mitaji, hatua itakayosaidia taasisi kukabiliana kwa ufanisi na mabadiliko ya mazingira ya biashara na teknolojia.

No comments