Ads

WAMILIKI WA ARDHI MKOA WA DAR WAHIMIZWA KULIPA KODI

Na Francisco Peter, Dar es Salaam 

Kaimu Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukran Kyando, amewaagiza wamiliki wa ardhi kulipa kodi ya pango la ardhi na kuendeleza maeneo yao ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

Maagizo hayo yametolewa leo jijini Dar es Salaam na Kyando, yakifuatia mkakati wa serikali wa kuwabana wadaiwa sugu na kuongeza makusanyo ya mapato.

Amesema kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wale watakaoshindwa kulipa kodi hiyo au kutotumia viwanja vyao ipasavyo. 

Aidha, wamiliki wa ardhi wametakiwa kutembelea Wizara ya Ardhi au ofisi za ardhi za mikoa ili kujua kiwango cha madeni yao na kulipa kwa wakati.

“Tayari tumekusanya asilimia 71 ya madeni, ambayo ni sawa na shilingi bilioni 63, huku lengo letu la kimkakati likiwa kufikia asilimia 100 ndani ya kipindi cha mwaka,” amesema Kyando.

Kyando ameongeza kuwa tayari wadaiwa takribani 600 waliochelewesha kulipa kodi hiyo wamepewa notisi ya kuwataka kulipa, na kabla ya kupewa taarifa hizo, walifanyiwa mazungumzo ya awali.

Aidha, amesema kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwigulu Rameck Nchemba, amekuwa akisisitiza umuhimu wa kufanya mazungumzo ya busara kabla ya kuchukua hatua za kisheria.

Ameeleza kuwa wamefikia hatua ya mwisho ya kuwaongezea wadaiwa muda wa wiki mbili zaidi kuanzia Aprili 24, 2026.

Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Thomas Lyapa, amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi kuhusu ulipaji wa kodi ya pango la ardhi kupitia televisheni, vipindi vya redio, matangazo ya gari (PA), pamoja na kufanya kliniki za ardhi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.


No comments