Ads

WANAHABARI WAKUMBUSHWA KUWA MASHUJAA UPATIKANAJI USAWA WA KIJINSIA

Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) kimewataka waandishi wa habari vijana kuwa mashujaa na mabalozi wazuri wa kusaidia upatikanaji wa usawa wa kijinsia kwa maendeleo ya nchi.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa chama hicho Dr. Mzuri Issa Ali wakati wa kufungua mafunzo ya siku tano ya kuendeleza waandishi wa habari vijana kuandika habari za uchambuzi juu ya wanawake na uongozi nchini.

Amesema kwa awamu hii vijana wa kiume wamepewa nafasi kubwa ambapo awamu ya pili waandishi wa kiume walikuwa sita tu lakini awamu hii jumla yao ni 10 ambao watashiriki katika mafunzo kwa lengo la kuwaanda kuwa vijana bora na wa mfano katika kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa wanawake kushiriki katika masuala ya uongozi.

“Vijana wa kiume haikuwa bahati mbaya kuwachagua bali tumefanya hivyo kuwajenga kuwa mashujaa, mabalozi na wanaume wa mabadiliko katika kuhamasisha usawa wa kijinsia kwa jamii”

Aidha Dr. Mzuri amaeongeza kuwa, tumechagua vijana wenye taaluma mbali mbali ikiwemo uandishi wa habari, waandaaji na waongozaji wa filamu ambao tunaamini watasaidia kuelimisha jamii masuala ya usawa wa kijinsia na wanawake kushiriki katika vyombo vya maamuzi.

Sambamba na hayo Mkurugenzi huyo amesema, lengo ni kuona ongezeko kubwa la ushiriki wa wanawake kugombea nafasi za uongozi kupitia mipango kazi itakayoandaliwa na vijana hao ambayo itazingatia uchambuzi wa takwimu na maazimio ya nchi yetu yenye kuridhia agenda ya dunia ya kufikia usawa wa 50% kwa 50%.

Nae Msanii na balozi wa habari Zanzibar Mustafa Yussuf, amewaomba baadhi ya wanaume kuondosha dhana potofu kwa wanawake katika uongozi na badala yake kuwasimamia ili kutimiza ndoto zao.

“Tumeona idadi ya wanawake viongozi inaongezeka, na ni waaminifu katika utendaji wao hata katika jamii ukilinganisha na wanaume," Mustafa alieleza.

Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA-ZNZ) imeandaa mafunzo kwa waandishi vijana 25 Unguja na Pemba ambapo wanawake jumla ni 15 na wanaume 10 kwa kushirikiana na Shirika (NED) la nchini Marekani.

No comments