WASANII WA FILAMU WAMPA "TANO" RAIS DKT. SAMIA
Na Francisco Peter
Wasanii mbali mbali kwenye tasnia ya filamu nchini washukuru hatua zinazofanywa na serikali ambapo wamejumuika kwa pamoja Kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kauli yake ya kuanza kuwajumuisha Wasanii mbalimbali kwenye ziara zake rasmi nje ya mipaka ya Tanzania kwa lengo la kujifunza zaidi juu ya tasnia hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 29, 2024 jijini Dar es Salaam Muigizaji na Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steve Nyerere amesema kuwa jambo hilo ni kubwa na wanazo sababu za kumshukuru Rais Samia.Rais Samia alitoa kauli yake ya kuanza kuwajumuisha Wasanii mbalimbali kwenye ziara zake rasmi nje ya mipaka ya Tanzania kwa lengo la kujifunza zaidi juu ya tasnia hizo hivi karibuni alipohudhuria hafla ya uzinduzi wa Albamu ya Staa wa Muziki wa Bongo Fleva Hamarmonize aliyoiita "Muziki wa Samia".
Amesema kuwa wao kama wasanii watahakikisha wanaitumia fursa hiyo katika kujifunza, kulinda maadili na kuitangaza Tanzania vizuri kiutamaduni na kiutalii jambo ambalo litaivuta Dunia kuifahamu vyema Tanzania.
Amesema Rais Samia anafanya hivyo kama mzazi anayepaswa kuwakumbatia watoto wake wote, ambapo ameleza kitendo cha Wasanii kupelekwa nje kujifunza kitawasaidia kuwainua kiuchumi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Waigizaji Tanzania Chiki Mchoma amesea kuwa kitendo hicho cha Rais Samia kinakwenda kuimarisha Tasnia ya Filamu Tanzania.
Aidha wasanii hao wametumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dkt. Samia kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kwa Tasnia nzima ya Sanaa, Utamaduni na Michezo.
Post a Comment