Ads

UFUGAJI HOLELA ULIVYOCHANGIA ONGEZEKO LA JOTO

Ng;ombe wa Maziwa 
Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Profesa George Msalya
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a.
Afisa Mkuu wa Utafiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Chirsker  Masaki.
.............

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Wafugaji wa Ng’ombe nchini wametakiwa kuzingatia kanuni za ufugaji ikiwemo idadi ya mifugo iendane na ukubwa wa eneo ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo ongezeko la joto inayochangiwa na wanyama kucheua na kutoa gesi inayoharibu utando wa anga (horizon layer) ambao unazuia uwepo wa jua kali nchini.

Akizungumza na mwandishi wetu jijini Dar es Salaam Msajili wa Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) Profesa George Msalya, amesema kuwa ongezeko la joto nchini imechangiwa na wafugaji kutozingatia utaratibu ikiwemo kuwa na idadi kubwa ya mifugo kuliko eneo la kufugia.

Profesa Msalya amesema kuwa uwepo wa mifugo mingi isiyofugwa vizuri inachangia gesi joto kutoka kwa wingi na kuharibu utandu unaozuia jua kali.

“Tanzania kuna ongezeko la joto, kumekuwa na mabadiliko ya hali ya hewa ya mara kwa mara ambayo imechangiwa na ufugaji ambao sio mzuri” amesema Profesa Msalya.

Profesa Msalya amesisitiza umuhimu wa kuzingatia  ufugaji wa kisasa unaozingatia viwango na kuangalia hali halisi ya mazingira ikiwemo kuwa na ng’ombe bora ambao wanakula chakula kidogo na kuleta mazao mengi.

Amefafanua kuwa ufugaji wa kisasa ni pamoja kufatilia taarifa za hali ya hewa na kuchukua tahadhari ya hali mbaya ya hewa ambayo imechangia kupoteza mifugo ya wafugaji ambao hawana utamaduni kufatilia taarifa za   Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).

“Taarifa za TMA zinawasaidia wafugaji kujipanga na kuona mbele yao kuna nini, kama kuna ukame wanajipanga kuifadhi malisho ya mifugo  pamoja na kutumia vizuri maji ili kuhakikisha wanatumia kwa muda mrefu” amesema Profesa Msalya.

Profesa Msalya amesema kuwa ni muhimu wafugaji kufuga kisasa ili kunufaika na fursa iliyopo katika sekta ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa kwani uzalishaji wa maziwa kwa mwaka lita bilioni 3.9, huku  uhitaji ukiwa lita bilioni 12. 

Ameeleza kuwa mwaka 2023 Serikali imetumia shillingi bilioni 23 kuagiza maziwa lita milioni 11 kutoka nchi zaidi ya 10 duniani ili kukizi mahitaji. 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema kuwa uboreshaji wa huduma za hali ya hewa umesaidia kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kisekta ikiwemo kilimo na ufugaji.

Dkt. Chang’a amesema usahihi wa utabiri unaotolewa na TMA umetokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika wa ununuzi na usimikaji wa mitambo ya kisasa ya uangazi na kuchakata pamoja na kuchambua taarifa za hali ya hewa.

Amesema kuwa serikali imefanikiwa kukamilisha ununuzi, ufungaji na mafunzo maalum ya matumizi ya kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuchakata data za hali ya hewa ili kusaidia seka mbalimbali pamoja na wafugaji.

TMA imefanikiwa kukamilisha mtandao wa jumla ya Rada saba (7) za hali ya hewa, ambapo katika kipidi cha miaka mitatu, malengo ya ununuzi wa Rada nne (4) yamefikiwa.

Afisa Mkuu wa Utafiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) Chirsker  Masaki, amesema kuwa wakati umefika kwa wafugaji nchini kufata utaratibu na ushauri wa wataalamu ili kuendana na mabadiliko ya hali ya hewa.

“Wafugaji wanapaswa kuzingatia ushauri wa sekta ya kilimo pamoja na kufatilia taarifa ya hali ya hewa ili kuleta tija na kufikiwa malengo yao” amesema Masaki.

No comments