AFRICA DAY MARATHON KUFANYIKA MIE 18, 2024, WANARIADHA WAJIPANGA KUSHIRIKI
Na Francs Peter, Dar es Salaam
Wanariadha wa Kitanzania ambao wameweka alama kimataifa, Juma Ikangaa, Alphonce Simbu, Filberty Bayi na wengineo watarajia kuwemo katika mbio ambazo zimepewa jina la Africa Day Marathon zinazotarajiwa kufanyika Mei, 18 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Mbio hizo ni maalumu kwa ajili ya mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini hususan waafrika kukimbia ikiwa ni kukumbuka kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (OAU) Mei 25, 1963, Adisababa nchini Ethiopia uliokuwa na lengo la kuzikomboa nchi ambazo hazikuwa huru kwa wakati huo.Akizungumza mbele ya waandishi wa habari leo, Mei 15, 2024 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika Mashariki Wizara ya Mambo ya Nje, Balozi Alli Bujiku amesema mbio hizo zitakuwa za kilometa 5 na 15 na zitahusisha mabalozi na baadhi ya maofisa wa kibalozi na watanzania kwa ujumla.
Balozi Bujiku amesema mbio hizo maalumu ni kwa ajili ya kuadhimisha miaka 61 ya kuanzishwa OAU mwaka 1963 na mwaka 2002 kubadilishwa jina na kuitwa (AU) baada ya nchi zote za Afrika kuwa huru na sasa wakiwa wanaangalia mafanikio na kupanga mikakati ya kusonga mbele na kujiletea mafanikio katika nyanja mbalimbali.
“Nchi nyingi za Afrika zinaadhimisha siku hiyo Mei, 25 kila mwaka, kwa Tanzania tunaadhimisha Mei 20, kutokana na Mei 25, 2024 kutakuwa na ugeni wa Baraza la Amani na Usalama,” amesema.
Pia ameongeza kuwa baada ya mbio hizo, watapeleka misaada katika shule zenye wahitaji maalumu nne, mbili zikiwa za Shule za Msingi na mbili za Sekondari ambazo ni Jangwani, Pungu, Uhuru Mchanganyiko na Jeshi la Wakovu.
Post a Comment