UTENDAJI WA RAIS DKT. SAMIA WAONGEZA UFANISI TMA
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imefanikiwa kufanya uboreshaji wa utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini.
Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na usahihi wa utabiri ambapo hivi karibuni tumeshuhudia madhara yatokanayo na mvua kubwa katika maeneo mbalimbali nchini, mvua ambazo zimechagizwa na uwepo wa hali ya El Nino.
Taarifa za uwezekano wa kutokea hali ya mvua kubwa ilitolewa TMA kupitia vyombo vya habari, ongezeko la usahihi wa utabiri huo uliotolewa kwa msimu wa VULI 2023 (Oktoba hadi Desemba kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka).
Usahihi umeendelea kuongezeka hadi kufikia asilimia 98% ambao ni kiwango cha juu zaidi ya asilimia 70 ya kiwango cha usahihi wa utabiri kinachokubalika kimataifa.
Mafanikio haya ni matokeo ya kazi kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha na kuboresha huduma za hali ya hewa hapa Nchini.
Katika kuonesha dhamira kwenye umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa, mara baada ya kutolewa tahadhari ya uwepo wa mvua kubwa, Mhe. Rais Dkt. Samia aliendelea kuwakumbusha wananchi kuchukua tahadhari kupitia ziara zake za kikazi Mkoa wa Manyara na Singida.
Ubora wa huduma za hali ya hewa umesaidia kuongezeka kwa tija na ufanisi katika mipango na utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kisekta, kuokoa maisha na mali kutokana na changamoto za matukio ya hali mbaya ya hewa.
Usahihi wa utabiri unaotolewa na TMA umetokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika wa ununuzi na usimikaji wa mitambo ya kisasa ya uangazi na kuchakata/kuchambua taarifa za hali ya hewa.
Mhe. Dkt. Samia amefanikisha kukamilisha ununuzi, ufungaji na mafunzo maalum ya matumizi ya kompyuta yenye uwezo mkubwa wa kuchakata data za hali ya hewa.
Kompyuta hiyo ni kisasa ya mfano katika ukanda wa Afrika, inaiwezesha TMA kuboresha shughuli za hali ya hewa hususani ongezeko la usahihi na uwezeshaji wa utabiri wa maeneo madogo madogo, huduma hiyo imeshaanza kufanyika ngazi ya wilaya kwenye utabiri wa msimu.
TMA imefanikiwa kukamilisha mtandao wa jumla ya Rada saba (7) za hali ya hewa, ambapo katika kipidi cha miaka mitatu, malengo ya ununuzi wa Rada nne (4) yamefikiwa.
Kati ya hizo Rada mbili zimeshafungwa katika Mkoa wa Mbeya na Kigoma, utengenezaji wa rada nyingine mbili zitakazofungwa katika mikoa ya Kilimanjaro na Dodoma unaendelea kiwandani nchini Marekani na zinatarajiwa kukamilika na kufungwa mwaka 2024.
Rada nyingine tatu (3) zilishafungwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Mtwara kupitia Serikali ya awamu ya nne na tano.
Hatua hii inaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Kikanda (Afrika Mashariki) kuwa na idadi kubwa ya rada za hali ya hewa saba (7), Uganda ikiwa na tatu (3) na Rwanda moja (1).
Maono ya Mhe. Dkt. Samia ni kuipa sekta ya hali ya hewa hadhi ya kimataifa, Mamlaka imenunua vifaa vya kuhakikia utendaji kazi wa vifaa vya hali ya hewa vinne (4) (Calibration Labaratory Equipments), vifaa hivyo ambavyo ni ya kisasa, vinaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika Mashariki na Kati kumiliki vifaa hivyo.
Serikali imeendelea kuwekeza katika usalama wa anga la nchi yetu kwenye upande huduma za hali ya hewa kwa kufanikisha ununuzi na kufungwa kwa vifaa vya kisasa vya hali ya hewa (Avimet) vinavyosaidia kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa ndege zinazoruka na kutua.
TMA ipo katika maadalizi ya ujenzi wa jengo la hali ya hewa pamoja na kituo cha kutoa tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa (Climate Analysis and Early Warning Centre) katika Jiji la Dodoma ambapo ujenzi umefika asilimia 38.
Kukamilika kwa ujenzi huo kutaimarisha utoaji wa huduma za hali ya hewa pamoja na mfumo wa kutoa tahadhari za matukio ya hali mbaya ya hewa nchini.
Hali ya hewa haina mipaka, hivyo hali ya hewa ya nchi moja inaweza kuathiri mwenendo wa hali ya hewa katika nchi nyingine.
Kupitia kazi kubwa ambayo imeendelea kutekelezwa na Mhe. Rais Dkt. Samia katika Diplomasia ya Uchumi na hata kupelekea kuteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya ushauri ya Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabia nchi (Advisory Board of the Global Centre on adaptation).
TMA imepewa jukumu la kudumu la kuiwakilisha nchi kiutendaji/kiufundi katika masuala ya hali ya hewa katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization – WMO).
Post a Comment