Ads

MCHUMI CHUO KIKUU MZUMBE AANIKA FURSA ZA MVUA MSIMU WA MASIKA 2024.


Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Idara ya Uchumi na Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Profesa Aurelia Kamuzora.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a akizungumza na waandishi wa habari tarehe 22/02/2024 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utabiri wa msimu wa mvua za masika 2024.
.........

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM

Baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ambazo zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi februari, 2024 na kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei, 2024.

Akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu kuhusu umuhimu wa mvua za msimu wa masika 2024 katika sekta ya uchumi nchini, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Idara ya Uchumi na Mwenyekiti wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) Profesa Aurelia Kamuzora, amesema kuwa  uwepo mvua nyingi  ni fursa kwa watanzania katika kufanya shughuli za kilimo kwani ni sekta ambayo inachangia utoaji wa ajira kwa asilimia 64.

Profesa Kamunzora amesema kuwa  kiuchumi mvua zinaleta fedha za kigeni kupitia kilimo cha kimkakati ikiwemo kahawa, pamba pamoja na korosho ambapo mazao yake hayahitaji umwagiliaji.

Uchumi huyo amesisitiza umuhimu kwa wakulima kutumia taarifa za TMA  katika utekelezaji wa kazi zao, huku akiwataka wananchi katika kipindi  cha mvua za masika kutengeneza miundombinu ya kuvuna maji ambayo yanaweza kuwa msaada katika kipindi cha ukame.

“Mvua zina faida kubwa katika uchumi kuliko hasara ambazo tumeziona ikiwemo uharibifu wa miundombinu; mfano zao la kahawa limeshika nafasi ya pili mwaka 2023 kwa kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni, na mwaka ujao tunatarajia kupata fedha zaidi kutokana na mvua kubwa ambazo zitachangia upatikanaji zao la kahawa ” amesema Profesa Kamuzora.

Ameeleza kuwa kwa sasa vijiji vingi wamelima zao la kahawa kutokana na uwepo wa mvua za kutosha, hivyo mwaka 2025 wanatarajia kupata  tani nyingi tofauti na mwaka 2023 ambapo walipata tani 80,000.

Profesa Kamuzora amesema kuwa teknolojia ya kilimo nchini bado inategemea mvua ili wakulima waweze kupata mazao ya kutosha, huku akieleza kuwa uwepo wa mvua ni neema katika utekelezaji wa shughuli za uchumi kupitia kilimo tofauti na baadhi ya watu wachache wanaotafsiri kama hasara hasa wanaoishi mjini.

“Miaka michache iliyopitia tulishuudia ukame katika maeneo mengi, tuliona mazao yakikauka, mifugo ikafa ilikuwa ni janga kubwa, lakini sasa mvua imeleta malisho ya mifugo na mazao yamestawi vizuri” amesema Profesa Kamuzora.

Profesa Kamuzora amesema kuwa mwaka ujao wakulima wanatarajia kupata mazao ya kutosha jambo ambalo litasaidia kupunguza mfumuko wa bei sokoni pamoja na kupata fursa ya kuuza mazao nje ya nchi na kupata fedha za kigeni ambazo zitachangia kukua kwa pato la Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana 22/02/2024 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa taarifa ya utabiri wa msimu wa mvua za masika, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema kuwa 

Mvua hizo zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), pwani ya kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani (ikijumuisha visiwa vya Mafia).

Mikoa mengine ni Dar es Salaam, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. 

Kanda ya Ziwa Victoria: (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kakonko na Kibondo).

Dkt. Chang'a amewashauri wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa wakati.

"Wakuliwa wanapaswa kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, mmomonyoko na upotevu wa rutuba, na kuchagua mbegu na mazao sahihi kwa ajili ya msimu huu wa Masika"  amesema Dkt. Chang’a.

Dkt. Chang'a amesema kuwa wafugaji na wavuvi wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa malisho na chakula cha samaki kupitia mvua za masika.

Ametoa tahadhari ya uwepo wa mlipuko wa magonjwa ya mifugo kama vile ugonjwa wa homa ya bonde la ufa na kuzaliana kwa wadudu wanaosambaza magojwa.."Matukio ya kuongezeka kwa magonjwa ya mwani baharini na kupungua kwa uzalishaji wa mwani kutokana na kupungua kwa kiwango cha chumvi ya maji ya bahari vinatarajiwa kutokea" amesema.

Amesisitiza kuwa jamii inashauriwa kuweka mipango mizuri ya matumizi bora ya maji na malisho pamoja na kufuatilia mirejeo ya tabiri za hali ya hewa na ushauri kutoka kwa maafisa ugani ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza na kuongeza tija katika msimu huu wa mvua za masika.

Dkt. Chang’a amesisitiza jamii kuendelea kufuatilia taarifa za mara kwa mara zinazotolewa na TMA kwa vile ni za uhakika, huku akibainisha kuwa usahihi wa msimu wa Vuli 2023 ulikuwa asilimia 98.

No comments