TFS YATAKIWA KUWEKA MIKAKATI YA MITI YA MATUNDA SHULENI.
Na Mwandishi Wetu, Mkinga
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe Dunstan Kitandula ameutaka uongozi wa wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) kuwa na mikakati ya kusambaza miche ya miti ya matunda katika maeneo ya shule za Msingi na Sekondari nchini.
Kitandula aliyasema hayo wakati wa ziara ya kutembelea shamba la miti Longuza na Hifadhi ya Msitu wa Asili Amani wilayani Muheza Mkoani Tanga ambapo aliutaka pia wakala huo kuanzisha vitalu vya malihai kwa wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari ili watoto na vijana wajifunze umuhimu wa uhifadhi wa maliasili za misitu nchini.
Aidha pia Kitandula ameutaka uongozi wa shamba la miti Longuza kuweka mkakati wa kusambaza zao jipya la miti inayozalisha zao la mpira kwa vijiji ambavyo vinazunguka eneo la shamba hilo kwa kuwapa elimu wananchi wajiunge kwenye kilimo cha miti hiyo.
Vilevile Mhe Kitandula ameitaka TFS kuboresha hostel na kuongeza vitanda kwa ajili ya watalii ambao wanahitaji kulala kwenye hifadhi ya Msitu wa Asili wa Amani ili kuunga juhudi za Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma katika sekta ya utalii.
Hata hivyo aliwataka viongozi wa shamba la miti Longuza na Hifadhi ya Msitu wa Asili Amani kuwaandaa wananchi na mkutano wa wadau wa mazao ya Nyuki utakaofanyika mwaka 2027 Jijini Arusha.
“Fursa za mazao yatokanayo na nyuki sio asali na Nta peke yake badala yake wafundisheni wananchi mazao mengine yanayotokana na ufugaji wa nyuki kwa ajili ya kunyanya kipato chao”Alisema
Awali akimkaribisha Naibu Waziri,Mkuu wa wilaya ya Muheza Mhe Juma Irando alimueleza kwamva moja ya changamoto inayowasumbua ni wananchi kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji ambavyo vipi katika Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Amani kwa ajili ya shughuli za kilimo pamoja na uchumbaji madini.
Mkuu huyo wa wilaya alitoa rai kwa Wakala huo wa Huduma za Misitu kuendelea kutoa elimu kwa zaidi ya uhifadhi katika msitu wa Amani ambayo ndio chanzo kikuu cha Maji yanayotumika Tanga na mji wa Muheza.
Post a Comment