TANZANIA NA MALAWI WASAINI MAKUBALIANO YA UTEKELEZAJI WA MRADI WA KUZALISHA UMEME
Waziri Wa Nishati, Mhe. January Makamba (kulia) akiwa na Waziri wa Nishati nchini Malawi Mhe. Ibrahim Matola wakisaini makubaliano ya pamoja ya ushirikiano katika kutekeleza miradi katika sekta ya Nishati na uzalisha umeme.
NA FRANCISCO PETER, DAR ES SALAAM
Serikali kupitia Shirika Umeme Tanzania (TANESCO) wameingia makubaliano ya ushirikiano katika kutekeleza miradi ya pamoja na Nchi ya Malawi sekta ya Nishati katika kuzalisha umeme.
Akizungumza leo Agosti 10, 2023 Jijini Dar es Salaam katika hafla ya kusaini Makubaliano ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Malawi, Waziri Wa Nishati, Mhe. January Makamba, amesema kuwa makubaliano hayo yanahusu ushirikiano katika maeneo ya uzalishaji wa umeme wa maji kupitia Mto Sogwe ambao upo pande mbili.
Mhe. Makamba amesema kuwa mradi huo utakuwa na megawati 300 ambao unakwenda kusaidia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Amefafanua kuwa pia wanakwenda kushirikiana katika kufanya tafiti na utafutaji wa gesi pamoja na ujenzi wa miundombinu ya umeme katika nchi hizo mbili.
"Katika utekelezaji wa makubaliano hayo tumeweka kamati ya wataalamu kwa pande mbili ili waweze kufatiliana kwa pamoja utekelezaji wake"
Kwa upande wake Waziri wa Nishati nchini Malawi Mhe. Ibrahim Matola, amesema kuwa ushirikiano huo unakwenda kuleta tija katika kuhakikisha wanafanya kazi kwa pamoja.
Amesema kuwa makubaliano hayo ni muhimu kutokana unakwenda kuzalisha umeme ambao unakwenda kuleta maendeleo baina ya Tanzania na Malawi.
Post a Comment