Ads

RAIS DKT. SAMIA AWEKA WAZI MIPANGO YA KUELENDELEA KUKOPA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kukopa mikopo yenye unafuu ili kufanya maendeleo.

Dkt. Samia amesema hayo wakati akipokea ripoti ya 2021-2022 za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


“Tupo vizuri labda ile asilimia 15% kwa 13% lakini tunatakiwa tusivuke hapo, mikopo ndio maendeleo, tutaendelea kukopa lakini tunakopa kwa akili,” amesema Dkt. Samia.

Hadi kufika Juni 30, 2022 deni la Serikali limeripotiwa kuwa ni kiasi cha Shilingi Trilioni 71.31 ikilinganishwa na kiasi cha Shilingi Trilioni 64.52 kilichoripotiwa mwaka wa fedha wa 2020-2021.

Kulingana na kiasi hicho, kumetajwa kuwa na ongezeko la Shilingi Trilioni 6.79 sawa na asilimia 10.5% ikilinganishwa na Shilingi Trilioni 7.79 sawa na asilimia 13.7% mwaka wa fedha uliopita.

Akisoma ripoti hiyo ya CAG mbele ya Rais Samia, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amesema katika mchanganuo huo wa deni hilo la Shilingi Trilioni 71.31, deni la Serikali linalojumuisha deni la ndani ni Shilingi Trilioni 24.04 na deni la nje ni Shilingi Trilioni 47.27 kwa mwaka wa fedha 2021-2022.

“Mwaka wa fedha 2020-2021, deni la ndani lilikuwa Shilingi Trilioni 18.93 na deni la nje lilikuwa Shilingi Trilioni 45.59 ambapo katika mwaka huo wa fedha (2020-2021) kulikuwa na jumla ya deni la Shilingi Trilioni 64.52,” amesema CAG Kichere wakati akisoma ripoti hiyo mbele ya Rais Samia.

Aidha, CAG Kichere amesema kipimo cha deni la Serikali kinachotumia pato la taifa, inaonyesha kuwa deni hilo la Serikali ni himilivu, kulingana na uwiano wa thamani ya sasa ya deni na mauzo ya nje kufikia asilimia 119.6% chini ya kikomo cha asilimia 180%.

Hata hivyo, CAG Kichere amesema uwiano wa kulipa madeni na mauzo ya nje nia asilimia 13.5% chini ya kikomo cha asilimia 15% sanjari na uwiano wa malipo ya madeni na mapato ni asilimia 14.1% chini ya kikomo cha asilimia 18%. 

No comments