Ads

TMA YATABIRI UWEPO WA MVUA ZA CHINI YA WASTANI HADI WASTANI MSIMU WA VULI

 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlala ya Hali ya Hewa nchini (TMA) Dkt. Agnes Kijazi akizungumza wakati akitoa Utabiri wa muelekeo wa msimu wa mvua za vuli (Oktoba hadi Desemba 2022),  jijini Dar es Salaam leo Septemba 2, 2022.


Pia vipindi vya joto kali kuliko kawaida vikitarajiwa katika msimu wa huu wa vuli hususani katika maeneo ya Pwani ya kaskazini na Nyanda za juu kaskazini Mashariki

Hayo yamesemwa leo Septemba 2, 2022 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlala ya Hali ya Hewa nchini (TMA) Dkt. Agnes Kijazi wakati akitoa Utabiri wa muelekeo wa msimu wa mvua za vuli (Oktoba hadi Desemba 2022), leo Septemba 2, 2022 jijini Dar es Salaam .

Hata hivyo Dkt. Kijazi amesema licha ya mvua hizo kuwa za chini ya wastani hadi wastani, pia kutakuwa na vipindi vya ongezeko kidogo la mvua katika maeneo machache hususan wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Disemba, 2022 na kwamba Kwa kawaida msimu wa mvua za Vuli huisha mwezi Disemba lakini kunatarajiwa kuwepo na mwendelezo wa mvua hizi hadi mwezi Januari, 2023.

Amesema, mvua za vuli zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba katika ukanda wa ziwa Victoria huku maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki na pwani ya kaskazini mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya nne ya mwezi Oktoba na wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2022.

Dkt. Kijazi ameitaja mikoa itakayopata mvua ya wastani na chini ya wastani kuwa ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Morogoro, Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Simiyu, Mara, mashariki mwa Mkoa wa Shinyanga na visiwa vya Unguja, Pemba na Mafia.

Mikoa mingine alisema ni ya kanda ya ziwa, ukiwamo Kagera, Geita, Mwanza na kaskazini mwa Kigoma itakayopata mvua za wastani na chini ya wastani.

Amesema upungufu wa unyevu wa udongo unatarajiwa kujitokeza maeneo mengi, hali inayoweza kuathiri ukuaji wa mazao na ongezeko la wadudu washambuliao mazao kama mchwa, viwavijeshi, panya pamoja na magonjwa ya mimea.

Dkt Kijazi ameshauri wakulima kupanda mazao yanayokomaa ndani ya muda mfupi na yanayostahimili ukame na watumie teknolojia za kilimo himilivu kuhifadhi unyevunyevu wa udongo.

Amesema mamlaka husika zinashauriwa kutoa ushauri kwa wakulima juu ya njia bora na namna ya kutumia kiwango kidogo cha mvua kinachotarajiwa kunyesha sambamba na matumizi mazuri ya akiba ya chakula kilichopo.

“Upungufu wa kina cha maji katika mito, mabwawa na hifadhi ya maji ardhini unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi na hivyo kuwepo uwezekano wa kupunguza upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali, ikiwamo uzalishaji wa umeme, lakini utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi utaendelea vizuri,” alisema.

Kwa upande wa menejimenti za maafa, zinashauriwa kuwa na usalama wa chakula, malisho ya mifugo, maji na kutoa miongozo ya namna ya kukabiliana na maafa ili kuzuia na kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

Pia Dkt. Kijazi amevishauri vyombo vya habari nchini kufuatilia na kusambaza taarifa sahihi za mwenendo wa hali ya hewa ili kufikisha taarifa hizo kwa wananchi kwa usahihi na wakati na kuweza kujikinga na madhara yanayoweza kujitokeza.

No comments