Ads

TIC YASAJILI MIRADI 274 KIPINDI CHA MWAKA 2021/2022.

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. John Mathew Mnali akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 17.8.2022 jijini Dar es Salaam kuhusu mafanikio ya TIC katika kipindi cha mwaka 2021/ 2022.

NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM.

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) katika kipindi cha mwezi Juni 2021 hadi Julai 2022 kimefanikiwa kusajili miradi 274 sawa na ongezeko la asilimia 14.6 ukilinganisha na mwaka 2020/2021 ambapo walisajili miradi 234.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 17.8.2022 jijini Dar es Salaam Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Bw. John Mathew Mnali, amesema kuwa miradi hiyo iliyosajiliwa inatarajiwa kuzalisha ajira 43,925 ukilinganisha na ajira 36,470 zilizoripotiwa katika kipindi cha mwaka 2020/2021.

Bw. Mnali amesema kuwa miradi hiyo ipo katika sekta za viwanda, kilimo, ujenzi, majengo ya biashara, miundombinu ya kiuchumi, taasisi za fedha, rasilimali watu, usafirishaji, utalii na huduma.

“TIC bado inaendelea kuhamasisha uwekezaji wa ndani nan je kwa kushirikiana na ofisi za kibalozi na ofisi za wakuu wa Mikoa, na serikali imeboresha mazingira ya uwekezaji kwa kuweka miundombinu wezeshi kama barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na umeme” amesema Bw. Mnali.

Bw. Mnali amesema kuwa kati ya miradi 274 iliyosajiliwa, miradi sita inatarajia kuwekeza kiasi cha dola za marekani bilioni 1.1 ambapo zitazalisha ajira za moja kwa moja 28, 710 na kuokoa fedha za kigeni zaidi ya dola za marekani bilioni moja ambapo zingetumika kuingiza bidhaa hizo kutoka nje ya nchi.

Amesema miradi hiyo ni pamoja na Itracom Limited kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea, Bagamoyo Sugar Limited inayojihusisha na kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari.

Miradi mengine ni Kagera Sugar Limited ambayo imejikita kwenye kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari, Mtibwa Sugar Estates ni mradi wa kilimo cha miwa cha uzalishaji wa sukari, Knauf Gypsum Limited inafanya shughuli za uzalishaji wa Gypsum powder na Gypsum board pamoja na mradi wa Gasi ambayo inafanya shughuli za uchakataji na usindikaji wa gesi.

Amebainisha kuwa serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha inarahisisha utoaji wa huduma kwa kuondoa urasimu, kutumia teknolojia ya mawasiliano, na kuweka vigezo vinavyotumika kutoa huduma.

Amesema kuwa serikali kupitia kituo cha uwekazaji imerahisishwa mfumo wa utoaji cheti cha Uwekezaji kwa kufanya maboresho ya utendaji kazi wa ndani (Business Process Engineering), mtiririko wa nyaraka na mfaili, utoaji maamuzi wenye tija.

“Serikali imeweka vigezo na viwango vya utaoaji huduma kwa wawekezaji, huduma zinatakiwa kwa wawekezaji ndani ya siku tatu kwa cheti cha uwekezaji, na kwa vibali vingine vyote vitoke ndani ya siku 14, kwa vibali wenye matatizo ya kisera serikali imeweka utaratibu wa wewekezaji wanapewa vibali vya muda” amesema Bw. Mnali.

Bw. Mnali amefafanua kuwa TIC katika mwaka 2022/2023 imejipanga kuendelea kuboresha mifumo ya kusajili ili kuongeza idadi ya miradi ya uwekezaji inayosajiliwa na kituo.

Pia wataendelea kuboresha na kuimarisha huduma zitolewazo katika kituo cha huduma za mahali pamoja (One stop Facilitation Center) ili kufanikisha uwekezaji, kuweka mikakati ya kufuatilia na kutathmini miradi ya uwekezaji iliyosajiliwa (Project Monitoring & Evalution).

“Tutaendelea kufanya tafiti mbalimbali ikiwa ni pamoja na tafiti za kuibua fursa za uwekezaji nchini, tafiti za kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa ajili ya wajasiramali wa kati na wadogo” amesema Bw. Mnali.

No comments