TAASISI YA RUFFO YATINGA MKOA WA PWANI KUWASAIDIA WANAFUNZI WA KIKE KUENDELEA NA MASOMO.
NA NOEL RUKANUGA, PWANI.
Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania imejipanga kuendelea kuwekeza nguvu katika kuzuia vitendo
vya ukatili wa kijinsia kwa watoto pamoja na kuhakikisha wanasoma katika
mazingira rafiki jambo ambalo litawasaidia kutimiza ndoto katika maisha yao.
Akizungumza hivi karibuni
Mkoani Pwani wakati akipokea msaada wa taulo za kike kutoka Taasisi ya Raising
Up Friendship Faundation (RUFF0), Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Mhe. Nickson
Saimon ‘Nikki wa Pili’ amesema kuwa wanaendelea kuwajengea uelewa wanafunzi
kuwa na uwezo wa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya ukatili kupitia program
mbalimbali.
Mhe. Saimon ameishukuru
taasisi ya RUFFO kwa kuleta taulo za kike katika Wilaya ya Kisarawe, kwani taulo
hizo zinakwenda kutatua changamoto kwa wanafunzi katika shule zenye uhitaji
wilayani humo.
“Nitakuwa sehemu ya
kampeni hii ya kuchangia taulo za kike na katika mikutano yangu nitalizungumzia
ili kuwasaidia wanafunzi wa keki kipindi ambacho wanapata hedhi wakiwa shuleni
wawe katika mazingira rafiki” amesema Mhe. Saimon.
Akizungumzia kuhusu
vitendo vya ukatili wilaya ya kisarawe, ameeleza kuwa idadi ya matukio ya
ubakaji yamepungua kwa asilimia kubwa, na hali hiyo imetokana na kufanikiwa
kuwakamata wahusika na kuwafikisha katika vyombo vya sheria kwa ajili ya kuchukuwa hatua.
Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Bw. James Chitumbi, amesema kuna baadhi ya
wanafunzi wapo katika mazingira magumu wakiwa katika kipindi cha hedhi kutokana na kushindwa kumudu gharama za taulo
za kike.
“Msaada wa taulo za kike unakwenda
kuwasaidia wazazi na wanafunzi wa kike wataona umuhimu wa kwenda shule bila
kuona aibu yoyote kwa sababu kuna vitu ambayo vinawaifadhi wakiwa katika
kipindi cha hedhi” amesema Bw. Chitumbi.
Ameeleza kuwa kutokana na
umuhimu wa jambo hilo halmashauri ya kisarawe wanapojenga miundombinu ya shule
wanatenga vyumba maalam vya wanafunzi wa kike kwa ajili kujiifadhi wakiwa
katika hedhi.
Amebainisha kuwa wakati
umefika serikali kutenga bajeti maalam kuwa ajili ya ununuzi wa taulo za kike
kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanapokuwa katika kipindi cha hedhi.
“Bajeti ikitengwa iwe na
usimamizi, inaweza serikali kuu ikatoa maagizo kwa halmashauri ya Wilaya itenge
asilimia ya fedha katika mapato yake kwa ajili ya kununua taulo za kike
kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji shuleni” amesema Bw. Chitumbi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya
RUFFO Bi. Hilda ngaja, amesema kuwa kupitia kampeni ya kuchangia taulo za kike wanaendelea kutoa msaada
katika shule mbalimbali zenye uhitaji kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kike
wakiwa katika hedhi.
Bi. Ngaja amesema kuwa lengo ni kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki ya
afya na uzazi na kuwasaidia kuepukana na changamoto ya kuomba ruhusa ya kwenda
nyumbani wakati wakipata hedhi.
“Tatizo
la hedhi linakuja kama dharura, hivyo taulo za kike zitawasaidia wakiwa shuleni
na kuepuka usumbufu wa kwenda nyumbani kipindi cha masomo” amesema Bi. Ngaja.
Amesema
kuwa katika Wilaya ya Kisarawe wamefanikiwa kwenda katika shule ya msingi na sekondari
ya Mfuru kwa ajili ya kuwapa wanafunzi
taulo za keki jambo ambalo litawasaidia
wakiwa katika hedhi shuleni.
Taasisi ya Raising Up
Friendship Foundation (RUFFO) inayopatika pia kupitia website ya
www.ruffo.or.tz inaendelea na kampeni ya kuchangia taulo za keki kwa
shule zenye wanafunzi wenye uhitaji katika Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na
Pwani.
Katika kuhakikisha wanazifikia shule zenye uhitaji wadau mbalimbali wametakiwa kuchangia kiasi chochote cha fedha kupitia namba ya MPESA 5447227 au kwa mawasiliano zaidi unaweza kupiga simu kwa namba 0765 670 746.
Post a Comment