SERIKALI KUWABANA WAMILIKI WA VYOMBO VYA USAFIRISHAJI WATAKAOKAIDI KUTOA MIKATABA KWA MADEREVA.
NA
NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema itaanza kuwachukulia hatua waajiri
na wamiliki vyombo vya Usafirishaji nchini ambao watabainika kukaidi maelekezo
ya kisheria (Compliance Order) ya kutoa mikataba kwa
wafanyakazi madereva ifikapo mwishoni mwa mwezi Agosti, 2022.
Hatua hiyo imekuja baada serikali kufanya ukaguzi katika
Mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Mwanza, Pwani na Mbeya ambapo imebainika jumla
ya Kampuni 73 zilikaguliwa na kubaini baadhi ya waajiri hawajatoa
mikataba kwa Madereva.
Akizungumza jijini Dar es
Salaam leo tarehe 22/7/2022 na waandishi wa habari, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi
ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Mhe. Patrobas Katambi, amesema kuwa kuhusu mishahara ya madereva kupitia benki, sheria ya ajira na mahusiano kazini, sura 366 imeruhusu mwajiri na mfanyakazi kukubaliana namna
ya kulipana mshahara ama kupitia benki, fedha taslim au hundi.
“Serikali inawashauri madereva kufanya makubaliano na waajiri wao kuhusu suala hilo. aidha, kupitia kaguzi zinazoendea kufanyika katika maeneo ya kazi, serikali itasimamia suala la madereva kupatiwa hati za malipo ya mshahara (salary slip) kama inavyoelekezwa kwenye sharia” amesema Mhe. Katambi.
Amesema kuwa kuhusu bima ya Afya, NSSF na Pensheni kwa Wastaafu, suala hilo lipo kwa mujibu
wa sheria ambayo inawataka waajiri wote kuwasajili na kuwachangia wafanyakazi wao katika
Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (NSSF na WCF) wakiwemo wafanyakazi madereva.
Ameeleza kuwa katika
ukaguzi uliofanyika awali ilibainika kuwa baadhi ya waajiri hawajawasajili madereva
wao katika mifuko hiyo, hivyo maelekezo ya kisheria yametolewa na serikali
itaendelea kufuatilia waajiri hao ili kuhakikisha wanatekeleza.
Mhe. Katambi
amefafanua kuwa kuhusu suala la matumizi ya Vidhibiti mwendo (Speed Governor) badala ya VTS; matumizi ya vidhibiti
mwendo yapo kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani sura 168 iliyofanyiwa
marejeo mwaka 2002.
“Katika kutekeleza Sheria hiyo, wamiliki wote wa
mabasi wameelekezwa kufunga vidhibiti mwendo kwenye mabasi yao ndani ya miezi 6
(kufikia Septemba, 2022). Serikali inatambua VTS kama kifaa halali cha
kufuatilia mwenendo wa mabasi, hivyo, Speed Governor na VTS vitaendelea
kutumika kudhibiti mwendo”
amesema Mhe. Katambi.
Katika hatua
nyengine amebainisha kuwa serikali
imetoa mwongozo wa kupakia na kushusha mafuta wa mwaka 2021 kwa wadau wote wa
usafirishaji wa mafuta (bohari za mafuta, wamiliki wa vituo vya mafuta, madereva
na wasafirishaji wa mafuta).
Amesema kuwa
ni jukumu la kila mdau kuhakikisha taratibu za upakiaji mafuta
zinafuatwa wakati akiwa katika bohari yoyote na
serikali itaendelea kutoa elimu kwa wadau wote ili waweze kuzingatia mwongozo
huu na hatua za kisheria zitachukuliwa kwa wadau watakaokiuka.
Utaratibu wa kusafirisha sumu, suala hili lipo kwa mujibu wa Sheria ya Kemikali za Viwandani na Majumbani Sura 182 ambayo imetoa mamlaka kwa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kusimamia wasafirishaji kwa kuwasajili wamiliki wa vyombo vya usafirishaji na kutoa mafunzo kwa Madereva wanaosafirisha sumu ndani na nje ya nchi.
Aidha, kwa mujibu wa
utaratibu imekubalika kuwa Vyeti anavyopatiwa Dereva baada ya kupatiwa mafunzo
kwa ufadhili wa Mwajini na Mali ya Dereva.
Hivyo, ili kuhakikisha
madereva hawalazimiki kupatiwa mafunzo wakiwa kazini,Serikali inaendelea na
hatua za kujumuisha mafunzo ya kusafirisha mafuta na kemikali hatarishi katika
mtaala wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ili kuwezesha kila Dereva
anayehitimu kuwana uelewa wa namna bora ya kusafirisha mafuta na kemikali
hatarishi.
Kuhusu ubovu wa magari, Serikali imetoa maelekezo
kwa Wakuu wa Vikosi vya Usalama Barabarani wa Mikoa (RTOs) kufanya ukaguzi wa
magari na kuchukua hatua kwa mujibu wa Sheria.
Aidha, Serikali kupitia Jeshi la Polisi na
LATRA inafanya jitihada za kuwa na Mfumo wa Ukaguzi wa lazima wa magari (Mandatory Vehicle Inspection) ambao
unatumia mitambo ya kisasa.
Kuhusu kuanzisha Kanzi Data ya Madereva; Sheria ya LATRA Namba 9 ya mwaka 2019 imeipa jukumu
Mamlaka kuwathibitisha Madaereva. Katika kutekeleza hilo, LATRA imetengeneza
Mfumo (Kanzi Data) ambao unawasajili Madereva
wote wa magari ya biashara.
Hadi kufikia Juni, 2022, LATRA imesajili zaidi ya
Madereva 10,236. Serikali inasisitiza Madereva waendelee kujisajili kwenye
Mfumo huo ili kukidhi matakwa ya Sheria.
Kuhusu hoja ya kuitisha vikao vya mashauriano ya wadau, Serikali
imepokea hoja hiyo na tayari imetekelezwa kwa kuitisha vikao vinavyoendelea.
Aidha, itaendelea kuitisha vikao hivyo kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu
ya kawaida bila kusubiri kuibuka kwa migogoro.
Kuhusu suala la Madereva
kujiunga na vyama vya wafanyakazi. Suala la kujiunga na vyama vya wafanyakazi ni la hiari kwa wafanyakazi.
Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Sura 366
inakataza waajiri kuwazuia wafanyakazi kujiunga na vyama husika. Serikali itaendelea kutoa elimu kwa Madereva na wamiliki wa Vyombo
vya Usafirishaji kuhusu umuhimu wa wafanyakazi kujiunga na vyama na kuchukua hatua kwa
waajiri watakaozuia Madereva kujiunga na vyama hivyo.
Kuhusu mabasi ya abiria kuingia kila kituo kwa safari za mikoani.
Serikali imeondoa vituo vilivyokuwa
vinalalamikiwa ambapo kwa sasa magari hayalazimiki kuingia katika kila kituo,
badala yake mabasi yataingia katika vituo vikuu. LATRA imeshatoa ratiba mpya
kutekeleza suala hili.
Kuhusu Maafisa Rasilimali watu na Maafisa Mahusiano kutotimiza wajibu wao, Kupitia kaguzi
zinazoendelea kufanyika katika maeneo ya kazi, elimu inaendelea kutolewa kwa
Maafisa husika ili kukuza uelewa wao
katika kusimamia rasilimaliwatu.
Pamoja na hatua zilizochukuliwa, ninawasihi Viongozi wa Vyama vya
Wafanyakazi wazingatie utaratibu uliowekwa kisheria katika majadiliano
ya kutetea maslahi ya wafanyakazi na kutatua migogoro ya kikazi.
Aidha, nitoe rai kwa Madereva wasio wanachama wa Vyama vya Wafanyakazi kuacha kutumia njia zisizo halali
kisheria kuanzisha au kuchochea vurugu
na migomo.
Vilevile, nitumie fursa hii tena kutoa maelekezo
kwa waajiri wote nchini kutekelezeza Sheria za Kazi na maagizo niliyoyatoa
ikiwa ni pamoja na kutoa mikataba ya kazi ili kujenga mahusiano mema sehemu za
kazi.
“Madereva na Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji, serikali ya awamu ya sita
inayoongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, itaendelea kushirikiana nanyi
kwa kuhakikisha kero na changamoto zinazoikabili sekta hii zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu” amesema Mhe. Katambi.
Serikali inatambua kwamba, kutozipatia ufumbuzi kero na changamoto katika sekta hii ni kurudisha nyuma jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali yetu katika kuhakikisha inaimarisha miundombinu ya usafirishaji nchini na kuvutia uwekezaji na mazingira bora ya biashara.
Post a Comment