Ads

MAJALIWA AKAGUA UWEKAJI ALAMA LOLIONDO, ATOA PONGEZI

 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezipongeza taasisi zote zilizokuwa zinaratibu zoezi la uwekaji wa alama katika eneo la pori tengefu la Loliondo kwa kukamilisha uwekaji wa vigingi 424 vilivyokusudiwa kuwekwa.

 

Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo (Alhamisi, Juni 23, 2022) alipotembelea eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1,500 kuona maendeleo ya uwekaji wa alama kuzunguka eneo la hifadhi.

 

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa eneo hilo lina umuhimu mkubwa kwa Watanzania na hata nchi jirani. “Hii ni tunu tuliyopewa na Mwenyezi Mungu, uwepo wa wanyama ni kivutio kikubwa kwa shughuli zetu za utalii, ni muhimu tuilinde.”

 

“Ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini unatokana na kodi ambazo Serikali inakusanya kutoka maeneo tofauti ikiwemo sekta hii ya utalii,” amesema Waziri Mkuu.

 

Amesema kuwa Watanzania hawana budi kuzingatia na kuzifuata sheria zilizowekwa. “Kila nchi ina utamaduni wake, hata wewe Mtanzania unapotoka kwenda nchi yoyote, fuata sheria za nchi hiyo.”

 

Amesema kuwa zoezi lililofanyika ni uwekaji wa alama tu, na hakuna mtu yeyote atakayeondolewa katika vijiji vinavyozunguka eneo hilo. “Hili eneo liko umbali wa karibu kilomita 12 hadi 15 kutoka kwenye makazi ya watu.”

 

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa zoezi la ulinzi katika eneo hilo ni endelevu katika kipindi chote na si wakati huu wa uwekaji wa alama pekee, na akaelekeza ulinzi uendelee kuimarishwa katika eneo la kilomita za mraba 1,500 zilizowekewa alama.

 

Naye, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana alisema kuwa eneo hilo ni muhimu katika sekta ya utalii na ni wajibu wa Wizara kuhakikisha eneo hilo linalindwa. “Tumeshapitisha GN, sasa itaitwa Pori tengefu la Pololeti la kilomita za mraba 1,500.”

 

Kwa upande wake, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bw. Mashimba Ndaki amesema kuwa Serikali inaendelea na ujenzi wa lambo kubwa litakalotumika kunyweshea mifugo katika eneo la Loliondo.

 

Alisema kuwa Serikali inajenga majosho 10 ya kuogeshea mifugo na tayari majosho mawili yameshakamilika huku mengine manane yakiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi. “Serikali inawajali na inawaangalia sana wafugaji,” alisisitiza.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Bw. Jumaa Aweso alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kupeleka huduma ya maji safi na salama katika maeneo yote nchini ikiwemo Loliondo.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,                                          

ALHAMISI, JUNI 23, 2022.

No comments