MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA UHURU NA MBINU MPYA.
SERIKALI ya awamu ya sita imekuja na mbinu mpya ya maandalizi ya maadhimisho ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika baadaye Tanzania.
Mbinu hiyo ni kuundwa kwa kamati ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya uhuru na kuweka utaratibu wa kukutana na waandishi wa habari kuanzia tarehe 1 hadi 30 Novemba mwaka huu.
Pia Wizara na taasisi mbalimbali zitakuwa zikielezea mafanikio ya maendeleo ya nchi tangu kupatikana kwa Uhuru hadi sasa.
Sambamba na hilo kamati hiyo imezindua nembo maalumu ya maadhinisho ya uhuru ambayo itatumiwa na vyombo vya habari na kauli mbiu isemayo "Miaka 60 ya Uhuru Tanzania Imara, Kazi Iendelee".
Akizindua nembo hiyo leo tarehe 1 Novemba, 2021 jijini Dodoma, Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ambaye ni Waziri Mkuu Majaliwa Kasimu Majaliwa, amesema maadhimisho hayo yanalenga kutoa elimu kwa jamii juu ya maendeleo baada ya kupata Uhuru.
Mhagama amesema kutokana na umuhimu wa maadhimisho hayo ambayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 9 mwaka huu, yatafanyika katika uwanja wa Uhuru Jijini Dar Es Salaam mahali ambapo Tanganyika wakati huo ilisherehekea uhuru mwaka 1961.
Amesema mgeni rasmi katika maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan.
"Shughuli za maadhimisho hayo zinaanza leo tarehe 1 Novemba, 2021 kwa Ofisi yangu kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu taswira nzima ya maadhimisho ya sherehe hizo za miaka 60 ya uhuru kitaifa" ameeleza.
Amesema katika maadhimisho hayo pia kutakuwepo mashindano ya insha kwa wanafunzi wa shule ya Msingi na sekondari, michezo kama vile mpira wa Miguu, kikapu, wavu, ridhaa na mashindano ya Baiskeli.
Aidha, Mhagama amesema tarehe 2 Desemba 2021 utafanyika uzinduzi rasmi wa juma la kilele cha sherehe za miaka 60 ya uhuru wa Tanzania bara.
"Uzinduzi huu utafanyika Jijini Dodoma na mgeni rasm anataraniwa kuwa Waziri Mkuu Kasim Majaliwa"
Post a Comment