Ads

Waziri mkuu Majaliwa atoa maagizo kwa mawaziri, azuia walinzi binafsi

 


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza Mawaziri na Naibu Waziri wasimamie taasisi na idara zilizopo chini ya wizara zao ili zizingatie vigezo vyote vya utawala bora pamoja na kukemesha vitendo vya rushwa ambavyo ndio adui mkubwa wa utawala bora.

“Ninapenda kuwakumbusha kuwa ninyi ni nyenzo muhimu katika utendaji wa Serikali, hivyo wazembe, wezi na wabadhirifu waliopo chini ya mamlaka zenu lazima wote wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Serikali. Kila kiongozi lazima awe makini muda wote.”

Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Ijumaa, Oktoba 29, 2021) wakati alipofungua Mafunzo ya Uongozi kwa Mawaziri na Naibu Mawaziri katika Ukumbi wa Mtakatifu Gasper jijini Dodoma. Mafunzo hayo yameandaliwa na Taasisi ya Uongozi.

Amesema lengo la mafunzo hayo ni kupanua uelewa wa Mawaziri na Naibu Mawaziri kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi ikiwa ni pamoja na kuelewa majukumu, madaraka na mipaka ya nafasi zao, kuongoza watu, kufanya maamuzi ya kimkakati na kuboresha sifa binafsi za kiuongozi.

Amesema ubadhirifu unatakiwa ushughulikiwe mapema kwa weledi na utaalam bila kulazimika kusimamisha utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa muda mrefu na hatua zichukuliwe bila kuoneana haya kama kuna ushahidi wa wazi kabla hata Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) hajakagua au viongozi wa juu kuchukua hatua.

Amewataka viongozi hao kutumia mada zitakazowasilishwa ili ziweze kuwasaidia katika kuzisimamia vyema Wizara wanazoziongoza na taasisi zilizo chini ya wizara zao ”mwende mkazisaidie taasisi hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake bila kikwazo chochote. Nendeni mkawe msaada kwao”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao kwa kushirikiana na Taasisi zingine waendelee kusimamia amani na utulivu kwenye maeneo yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote. “Amani na utulivu ndiyo itatuwezesha kama nchi, tuendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza mitaji yao hapa nchini.”

“Tunakumbushwa sisi viongozi wa Tanzania tuwe wazalendo na tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote bila ubaguzi wa jinsia, kabila, dini na rangi ili mradi mtu hajavunja sheria. Tuwahudumie Watanzania wote kwa usawa.”

Pia, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi hao waepuke matumizi ya walinzi binafsi na waandishi wa habari binafsi katika Ofisi za Umma kwani wanaweza kuwa  chanzo cha uvujaji wa siri za Serikali. “Upo utaratibu wa kufuata endapo itabainika mnahitajika kupatiwa wasaidizi hao. Zingatieni utaratibu huo na si vinginevyo.”

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Management ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa ameiagiza Taasisi ya Uongozi ihakikishe inaendelea kuandaa mafunzo ili kujadili masuala mbalimbali kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini, hususan ile inayosimamiwa na Ofisi ya Rais.

“Nia ni kutoa ujuzi, maarifa na taarifa kwa viongozi kutoka kwenye sekta mbalimbali juu ya umuhimu wa miradi hii. Kutokana na umuhimu wa miradi ya kimkakati, mikutano hii ni ya lazima.”

Pia, Waziri Mchengerwa ameziagiza wizara, idara na taasisi zote za Serikali zihakikishe zinatenga bajeti kwa ajili ya kuwapeleka watumishi viongozi kushiriki katika mafunzo yanayoandaliwa      na kutolewa na Taasisi ya Uongozi ili kuwaimasha kiutendaji.

No comments