Ads

DIT YAPONGEZWA KWA UBUNIFU SHUGHULI ZA KITAALUMA.

 

Msajili wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT)  Bw. Roy Elineema akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Wasichana Harrison UWATA ya Mkoani Mbeya walipotembelea taasisi hiyo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali.

.......................

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Wasichana Harrison UWATA ya Mkoani Mbeya wameishukuru Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kwa kuwapokea na kuwaonesha ubunifu pamoja na shughuli za kitaaluma zinazofanyika chuoni hapo.

Hatua hiyo ya pongezi imekuja baada ya kutembelea Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT)kwa ajili ya kujifunza fani mbalimbali zitolewazo.

Akizungumza na wanafunzi hao Msajili wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam Bw. Roy Elineema, amewapongeza wanafunzi hao kwa kuchagua kuitembelea  Chuo cha DIT.

Amesema kuwa kuitembelea DIT wamepata mwanga juu ya fani zinazotolewazo  ambazo pamoja na ziara hiyo, wakirudi shuleni kwao, watajua ni masomo yapi ya kutilia mkazo hasa wanaotaka kusoma fani za Uhandisi 'Engineering'.

"DIT ni Taasisi kongwe ya elimu ya  ufundi nchini na maarufu kwa fani za uhandisi na teknolojia na ili upate nafasi ni lazima uwe na ufaulu wa masomo manne ambayo ni Hesabu,Fizikia, Kemia na  hivyo, ni matumaini yangu kuwa kwa uelewa huu sasa mtafanya bidii kwenye eneo hili" amesema Bw. Elineema.

Mkuu wa Idara inayosimamia mafunzo viwandani  Dkt.John A. Msumba amesema kuwa DIT inafanya kazi kwa karibu na wadau wa viwandani ili kuhakikisha wanatoa wataalam wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira.

Dkt. Msumba amesema kuwa DIT inashirikiana na wadau wa viwandani ili kusaidia kutoa wataalam wenye ujuzi sawa na kile kinachofanyika viwandani, “Mwanafunzi anajifunza darasani na anaenda kujifunza kwa vitendo zaidi kiwandani"   

Mkuu wa msafara Mwl. Rainery Kayombo, ameishukuru DIT kwa mapokezi mazuri waliyoyapata, pia aliishukuru taasisi hiyo kwa utaalam waliowapatia wanafunzi wake.

Ameeleza kuwa ziara hii ya wanafunzi 81 imewafungua macho wanafunzi wao kwa kuwa wameielewa DIT na wameona namna ambavyo kazi za kitaaluma zinavyofanyika kwa vitendo na  namna ambavyo DIT imewekeza miundo mbinu katika fani wanazosoma.

No comments