Ads

DC BULEMBO Awataka Wananchi Wajiandae Na Sensa

  


Raisa Said,Muheza Tanga.

Mkuu wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga Halima Bulembo amewataka Wakazi wa Wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kuhesabiwa mchakato wa Sensa ya Watu na Makazi utakapoanza mwakani.


Akizungumza Wakati wa Ziara yake ya kujitambulisha na kuhamasisha shughuli za maendeleo,Bulembo alisema suala la kuhesabiwa ni muhimu sababu Serikali haiwezi kutengeneza mipango ya maendeleo kwa wananchi wake bila kuwa na takwimu sahihi za wakazi wa eneo husika.


Akifafanua, Bulembo alieleza kuwa lengo la sensa hiyo ni kuisadia Serikali kupata taarifa za msingi zitakazosaidia mchakato wa utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025, mageuzi ya masuala ya afya na jamii, pamoja na ufuatiliaji wa ajenda za maendeleo za kimataifa.


Alisisitiza kuwa taarifa za idadi ya watu husaidia katika mamlaka za wilaya katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ambayo huakisi matakwa ya watu katika ngazi husika na kusaidia kwenye uwiano wa mgawanyo wa rasilimali


"Takwimu sahihi za Sensa zinahitajika kwa ajili ya ugawaji wa majimbo ya uchaguzi kwa ufanisi, kurekebisha mipaka ya kiutawala katika serikali za mitaa" Alieleza Bulembo


Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya huyo alisema kama wilaya wamejipanga kuendelea kuihamasisha jamii kwenye mikutano ya hadhara na Vikao kwenye ngazi ya Wilaya, Kata, Vijiji na Vitongoji ambapo ajenda ya Sensa inatakiwa kuwa ya Kudumu.


Alisema kuwa wilaya itatumia vipeperushi na mabango pamoja na kutumia taasisi zilizopo kama shule na vyuo kutoa elimu kwa wanafunzi.


Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 wilaya ya Muheza ilikuwa na idadi ya watu 204,461. Kati ya idadi hiyo, wanaume ni 100,843 (asilimia 49.3) na wanawake ni 103,618 (asilimia 50.7)).


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepanga kufanya Sensa ya Watu na Makazi ifikapo mwezi Agosti 2022.


Wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar (OCGS), ipo kwenye maandalizi ya kufanya Sensa hiyo.


Sensa ya Watu na Makazi ni zoezi la kitaifa linalofanyika kila baada ya miaka 10 ambapo Sensa ya mwisho kufanyika nchini ni ile ya mwaka 2012.


Hivyo Sensa ya mwaka 2022 itakuwa ni sensa ya Sita kufanyika nchini baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.


No comments