Ads

TUMIENI WATAALAMU WA NDANI KUANDAA MIPANGO KABAMBE-NAIBU WAZIRI MABULA

 
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akionesha Mpango Kabambe wa Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa tarehe 19 Julai  2021 baada ya kuuzindua alipokuwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi.

Naibu Waziri wa Ardhi nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametoa rai kwa mamlaka za upangaji nchini kuandaa mipango kabambe ya maeneo yao kwa kutumia wataalamu washauri au wataalamu wa ndani kadri ya uwezo wa mamlaka husika.

Aidha, amezielekeza halmashauri ambazo zimeanzisha mchakato wa kuandaa Mipangop Kabambe kuongeza jitihada kukamilisha kazi hizo na wataalamu watekeleze majukumu yao kwa weledi.

Naibu Waziri Mabula alitoa rai hiyo tarehe 19 Julai 2021 wilayani Sumbawanga wakati akizindua Mpango Kabambe wa Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa.

Alisema, mipango kabambe inaongeza kasi ya kupanga na kupima miji yetu sambamba na kuondoa changamoto mbalimbali zikiwemo za migogoro ya matumizi ya ardhi , ukuaji wa makazi yasiyo rasmi , uharibifu wa miundombinu  na mazingira,  kukuza fursa za uwekezaji pamoja na kuongeza ajira kwa wananchi wa manispaa ya Sumbawanga.

‘’ kama tunavyojua Tanzania imepimwa kwa kiwango kisichozidi asilimia 25 na kama tumeenda mbali tunasogea asilimia 30 lakini tunavyoendelea kuweka mipango midogomidogo kulingana na mamlaka husika tutajikuta tumepnga nchi nzima na wizara ya ardhi imejipanga katika hilo’’ alisema Dkt Mabula.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, kukamilika kwa Mpango Kabambe wa Manispaa ya Sumbawanga kumekuja wakati muafaka maana pamoja na kutumika kama chombo cha kuongoza na kusimamia uendelezaji mji pamoja na kudhibiti  ujenzi holela pia utatoa uhakika wa uwekezaji kwenye halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga..

Alitoa wito kwa halmashauri zote nchini ambazo hazijaandaa Mipango Kabambe ya miji yao kuiga mfano wa Manispaa ya Sumbawanga ili kuongeza kasi ya kupanga na kupima miji yote nchini.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, hadi sasa kuna jumla ya mipango kabambe 26 iliyoandaliwa katika mamlaka za upangaji na kuidhinishwa na wizara na zoezi la kuizindua linaendelea. Hata hivyo, tayari mipango kabambe ya jiji la Dodoma, Manispaa za Mtwara Mikindani, Musoma , Iringa, Singida , Tabora na Miji ya Njombe na Tunduma imekamilika na kuzinduliwa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisema, Mpango Kabambe wa Manispaa yake utekelezaji wake upo katika awamu nne za miaka mitano mitano ambapo jumla ya miradi 12 ilitarajiwa kutekelezwa katika awamu ya kwanza (2015/2020) na baadhi yake ni kituo cha mabasi Katumba, kufungua miji ya pembeni pamoja na mpango wa urasimishaji makazi holela

No comments