WANUFAIKA 395 WA MKURABITA MUFINDI WAFURAHIA MAFUNZO YA KUWAINUA KIUCHUMI
Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), Anthony Temu akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo kiuchumi wanufaika wa mpango huo waliorasimishiwa ardhi yao kwa kupatiwa hati miliki za kimila katika Kijiji cha Lugodalutali Kata ya Igombavanu, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, mkoani Iringa Juni Mosi, 2021.
Walioshiriki mafunzo hayo walikuwa 395 ambapo walifundishwa jinsi ya kutumia hati miliki kuweka kama dhamana kukopea fedha benki na taasisi zingine za fedha ii kuinua mitaji ya miradi yao, kanuni bora za kilimo ili kupata mavuno mengi kwa heka moja, kuthaminisha rasilimali zao na hasa ardhi, jinsi ya kuweka kumbukumbu za mahesabu ya miradi yao, umuhimu wa kujiunga na ushirika na faida zake na faida za kuweka akiba benki na mikopo inayotolewa na benki hizo.
Pia walifundishwa jinsi ya kufuga nyuki na mazao yake ikiwemo asali, nta, chavua, sumu ya nyunki na thamani yake kwenye masoko. Wakati wa mafunzo hayo kikundi cha watumia maji walikabidhiwa msaada wa mizinga 30 iliyotolewa na Mkurabita.
Maofisa walioshiriki kutoa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Meneja Urasimishaji Ardhi Vijijini wa Mkurabita, Anthony Temu ni;Maofisa wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi ambao ni Afisa Ardhi Mteule, Leonard Jaka, Afisa Ushirika, Pili Mwaipaja, Afisa Kilimo, Mwamini Mwakyaka, Afisa Ufugaji Nyuki, Hamisi Hassan,Afisa Maendeleo ya Jamii, Joha Kambala na Afisa Upimaji Ardhi Imamu Sherukindo.
Kwa upande wa benki waliotoa mafunzo ni Meneja Biashara wa Benki ya CRDB, Gasper Mlala, Afisa Mikopo wa Benki ya Posta, TPB, Japhet Peter na Prosper Peter wa Benki ya Mucoba ambao kila mmoja alieleza masharti ya kujiunga, masharti ya ukopaji na faida zake. Benki zote hizo zinaruhusu kuweka hati miliki za kimila kuweka kama dhamana kukopa fedha.
Awali mafunzo hayo ambayo wengi waliyafurahia na kuomba Mkurabita kuwapelekea tena siku nyingine, yalifunguliwa na Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Sailas Kiwuyo na kupata baraka za mgeni rasmi ambaye ni Diwani wa Kata ya Igombavanu,Veronica Kilongumtwa.
Post a Comment