MADIWANI WAWAVIMBIA WATENDAJI WALIOWASABABISHIA HATI YENYE MASHAKA KISHAPU
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu wakipitia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, na kujadili hoja zilizotolewa 119 na kupata Hati yenye Mashaka.
Na Marco Maduhu, Kishapu
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, wamejadili hoja Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, na kuazimia kuchukuliwa hatua watendaji ambao wamewasababishia kupata Hati yenye Mashaka.
Maazimio hayo yametolewa leo kwenye kikao maalumu cha baraza la Madiwani, lililokuwa na ajenda ya kujadili hoja za CAG katika mwaka wa fedha 2019-2020.
Awali akisoma taarifa hiyo ya CAG Mkaguzi wa ndani wa Halmashauri ya Kishapu Florence Kuruletera, alisema Halmashauri hiyo ina hoja 119, ambapo hoja 68 ni za kipindi cha nyuma, na 51 niza mwaka wa fedha 2019-2020, ambapo kati ya hoja zote hizo 38 zimeshafanyiwa kazi, na 41 zipo hatua ya utekelezaji, 40 bado hazijatekelezwa.
Alisema kutokana na kuwepo kwa hoja hizo, Halmashauri hiyo katika mwaka huo wa fedha 2019-2020 imepata Hati yenye Mashaka, huku baadhi ya sababu zilizosababisha ni ukosefu wa nyaraka za malipo, na udhaifu wa ukusanyaji mapato.
Aidha kufuatia kuwepo na hoja 119 huku nyingine zikijirudia kila mwaka, Madiwani hao kwa pamoja waliazimia kuwa watumishi wote ambao wamesababisha kupatikana kwa hoja hizo sababu ya uzembe wawajibishwe, pamoja na kuzirudisha fedha ambazo walikosa viambatanisho vya malipo.
Mmoja wa Madiwani Lucas Mkende wa kata ya Mwamashele, alisema haiwezekani wao kuchafuliwa kwa kupata hati yenye mashaka kwa sababu ya baadhi ya watumishi ambao ni wazembe, na kueleza kuwa ni vyema wakawajibishwa ili kusijirudie kwa hoja za mara kwa mara.
Naye Baraka Bulongo kutoka Ofisi ya Katibu Tawala msaidizi upande wa Serikali za Mitaa, alisema mtumishi ambaye amelipwa na kushindwa kuwasilisha vielelezo ndani ya siku 14, anapaswa kuwajibishwa na hata kukatwa pesa hiyo kwenye mshahara wake.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Kishapu William Jijimya, aliwaonya watendaji wa Halmashauri hiyo na kuwataka kufuata miongozi na kanuni za kazi ,ili kutosababisha upatikanaji wa hoja nyingi.
Alisema kwa watendaji wale ambao wameisababisha Halmashauri kupata hoja nyingi na Hati yenye Mashaka sababu ya uzembe, hawatakuwa na msamaha nao bali watawajibishwa ilikuwa fundisho kwa wengine.
Post a Comment