Ads

Waziri Mwigulu Nchemba Atoa Maagizo kwa Msajili wa Hazina


Na Mwandishi Maalumu, Arusha
WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amemuelekeza Msajili wa Hazina kufanya tathmini ya utendaji na ufanisi wa Taasisi na Mashirika ya Umma ili aje na ushauri mzuri kwa Serikali ikiwemo kupendekeza kufutwa na kuunganishwa kwa baadhi ya taasisi au kuanzishwa kwa taasisi mpya kama kutakuwa na ulazima huo. 


“Hii itasaidia serikali kubaki na taasisi na mashirika yenye kuleta tija badala ya kuwa mzigo kwa serikali,” ameeleza.


Aidha, amesema hatakubali kuona taasisi, mashirika ya umma na wakala za serikali zinashindwa kuwasilisha hesabu zake kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka huu, huku akianisha maeneo 10 ambayo wanatakiwa kuyawekea msisitizo na kuimarisha mifumo ya utendaji na uwajibikaji wa taasisi ili zitoe huduma sahihi na endelevu.


Dk Mwigulu aliyasema hayo jana jijini hapa wakati akifungua mafunzo ya mikataba ya utendaji kazi ya Ofisi ya Msajili wa Hazina na bodi za taasisi, mashirika ya umma na wakala za serikali yanayofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC).


Katika hotuba yake iliyosomwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Khatibu Kazungu, Dk Mwigulu alisema serikali imefanya uwekezaji wa takriban Sh trilioni 65 kwenye taasisi na mashirika yapatayo 237 kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali za kijamii, kiuchumi na kusaidia katika kuchangia Pato la Taifa. 


“Ni vyema mkafahamu kwamba taasisi na mashirika haya yanatumia kiasi kikubwa cha fedha za umma kwa njia ya mitaji, mishahara na matumizi mengineyo. Kwa misingi hiyo ni matarajio ya Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kwamba, taasisi na mashirika haya yatasimamiwa ipasavyo ili yaweze kutoa huduma sahihi na endelevu,” alisema Dk Mwigulu.


Aliongeza kuwa pamoja na jitihada zinachokuliwa na serikali, bado kuna maeneo 10 ambayo ni muhimu kuweka msisitizo wa kuimarisha mifumo ya utendaji kazi na uwajibikaji wa taasisi hizo.


Aliyataja kuwa ni baadhi ya taasisi bado zinachelewa kuwasilisha hesabu za taasisi kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa ajili ya ukaguzi. “Katika mwaka huu wa fedha na miaka ijayo sitapenda kusikia tena taasisi yoyote ya umma kwamba imeshindwa au kuchelewa kuwasilisha hesabu kwa wakati,” alieleza.
 
“Aidha, taarifa hizo (za utekelezaji za robo mwaka na mwaka) zinazowasilishwa kwa Msajili wa Hazina ni lazima zipitiwe na kumilikiwa na uongozi wa taasisi,” alibainisha na kumuagiza Msajili wa Hazina kuchukua hatua stahiki kwa watakaoshindwa kutekeleza hilo.


Jingine ni kuagiza taasisi na mashirika yote kuhakikisha matumizi yao yanazingatia Mwongozo wa Bajeti wa Mwaka 2021/22 na kanuni zake zinafuatwa ipasavyo katika utekelezaji wa bajeti.


“Na kwa taasisi na mashirika ambayo hazikuzingatia mwongozo wa bajeti hususan kwa fedha za maendeleo, nakuagiza Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango mzichambue upya na kusitisha miradi yote itakayoshindwa kukidhi matakwa ya mwongozo wa Bajeti kwa mwaka 2021/22,” aliagiza.

No comments