WANANCHI TUNDURU WATAKIWA KUTUMIA VYEMA UJUZI WA KUKABILIANA NA TEMBO
Wananchi waliopewa mafunzo ya kukabiliana na tembo wakionyesha kwa vitendo namna ya kutumia wigo wa pilipili na oili chafu ili kumfukuza tembo aliyevamia makazi ya watu onesho lililofanyika katika kijiji cha Jakika Wilayani Tunduru jana.
*************************
Na Happiness Shayo -TUNDURU
Wananchi 20 kutoka vijiji vya Wilaya ya Namtumbo na Tunduru waliopewa mafunzo ya ulinzi wa wanyamapori na namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu kama tembo wametakiwa kuhakikisha wanautumia vizuri ujuzi huo ili kuilinda jamii inayokabiliwa na tatizo la kuvamiwa na tembo.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius Mtatiro wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyama waharibifu kama tembo yaliyofanyika katika ukumbi wa Klasta Wilayani Tunduru jana.
“ Ndugu zangu ambao mmekuja kwenye haya mafunzo msiende kuyaweka kabatini, muende mkayafanyie kazi na mkatoe elimu kwa wananchi na mtumie mafunzo haya kuwadhibiti wanyama waharibifu ” Mhe. Mtatiro amefafanua.
Aidha, amewaasa wakufunzi hao kuwa wepesi kutoa taarifa za uvamizi wa wanyamapori waharibifu katika makazi ya watu pindi inapotokea.
“Nimewakamata wenyeviti kadhaa wanaochukua rushwa na kuruhusu ng’ombe kuingia hifadhini, lakini hii haitasaidia isipokuwa tu pale ambapo mtaamua kutoa taarifa kwa watendaji wa vijiji na ofisi ya mkuu wa wilaya mnapoona makundi ya ng’ombe hifadhini” Mhe. Mtatiro amesema.
Mhe. Mtatiro amewaagiza wakufunzi hao kuhakikisha wanawaelimisha wananchi wengine juu ya mbinu mbalimbali walizojifunza za namna ya kukabiliana na wanyama wakali na waharibifu na pia kuzalisha watu wengi kwenye maeneo yao ambao wana weledi wa udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu ili jamii ibaki salama.
Akizungumza kwa Niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Wanyamapori (TAWIRI), Dkt. Janemary Ntalwila amesema kuwa mafunzo hayo yamejikita katika kuelezea njia rafiki za kukabiliana na uvamizi wa tembo.
“ Njia zitakazotumika ni njia rafiki na za gharama nafuu kwa mfano matumizi ya mabomu ya pilipili , tochi maalum za kufukuzia tembo, fataki, honi, mizinga ya nyuki, uzio wa vitambaa vilivyolowekwa kwenye mchanganyiko wa oili chafu na pilipili ” Dkt. Ntalwila ameongeza.
Dkt. Ntalwila amesisitiza kuwa, njia hizo zikitumika ipasavyo zitasaidia kuboresha maisha ya wananchi kwa kusaidia kuongeza kipato akitolea mfano matumizi ya njia ya mizinga ya nyuki ambayo ina uwezo wa kufukuza tembo na pia kutoa asali, nta na gundi ya nyuki.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Wanyamapori kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Silvanus Okudo amesema mafunzo hayo yatasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la uvamizi wa tembo.
”Nia ya Serikali ni kuisaidia jamii kupunguza au kuondokana kabisa na tatizo hili la kuvamiwa na wanyama wakali na waharibifu na tunaamini kuwa wakufunzi hawa watajitahidi kuzuia changamoto hiyo kabla haijajitokeza” amesema Bw. Okudo.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Amiri Abeid ambaye ni Mkazi wa Kijiji cha Libangu Wilaya ya Namtumbo amesema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha wanavijiji kuwadhibiti wanyama wakali na waharibifu pindi wanapovamia makazi yao.
“Lengo la mafunzo haya ni kutuwezesha namna ya kuishi na kukabiliana wanyama wakali na waharibifu kama tembo lakini pia kuchukua ujuzi na kwenda kuwafundisha wanavijiji wengine” amesema Bw. Abeid.
Mafunzo ya kudhibiti wanyama wakali na waharibifu yamehudhuriwa na wakufunzi ishirini kutoka vijiji vya Wilaya ya Namtumbo na Tunduru na yameandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA)
Post a Comment