Maxence Melo Mkurugenzi wa Jamii Forums, Ahukumiwa Kifungo cha Nje
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja, Mkurugenzi wa Jamii Forums, Maxence Melo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kuzuia Askari Polisi kutekeleza majukumu yake.
Mahakama hiyo pia imemuachia huru mshitakiwa Mike Mushi kutokana na upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yake, huku ikimuonya Melo kutofanya kosa lolote ndani ya mwaka mmoja.
Hukumu hiyo imesomwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Faraji Ngukah.
Katika hukumu hiyo, Hakimu Shaidi amesema mahakama inamuhukumu Melo kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya kutiwa hatia kwa kosa la kuzuia Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu, pia inamuachia huru Mushi ambaye alionekana kama msindikizaji katika kesi hiyo.
Hukumu hiyo imetolewa baada ya Upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao kwa kuleta mashahidi sita huku Melo akijitetea mwenyewe bila kuwa na shahidi mwingine.
Awali kabla ya kusomwa hukumu hiyo Wakili Faraja Ngukah ameiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa kwani kitendo alichokifanya cha kuzuia askari kutekeleza majukumu yao ni hatari kwa Taifa.
Hata hivyo, Wakili wa utetezi, Bernedict Ishabakaki ameiomba mahakama itoe hukumu ya faini kwa sababu washitakiwa ni vijana ambao wameajiri na wanategemewa.
Post a Comment