Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga awatuliza wananchi baada ya Sungusungu Kuzua taharuki na kupora watu fedha.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mh. Carolius Misungwi ameagiza kusimamishwa kwa shughuli za Sungusungu katika kata ya Mfinga iliyopo bonde la ziwa Rukwa, Wilayani Sumbawanga baada ya Sungusungu hao kuzua taharuki baada ya kuwazuia wanakiijiji kuendelea na shughuli zao na kuwakusanya uwanjani na kuwanyang’anya fedha pamoja na kutoa adhabu kwa waliogoma kutii amri zao.
Mh. Misungwi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya amemuagiza Kamanda wa Polisi Wilaya ya Sumbawanga Pamoja na Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya kuhakikisha wanafika katika Kijiji hicho na kukutana na uongozi wa Sungusungu wa Kata na wa Kijiji ili kuwapa elimu juu ya namna ya kufanya shuguli za ulinzi shirikishi kwa taratibu zinazokubalika kisheria na sio kujichukulia sharia mkononi.
“Kuanzia leo nimesimamisha shughuli zote za Sungusungu mpaka atakapokuja OCD kutoa mafunzo ya namna ya kufanya ulinzi shirikishi, na tungependelea sana kuwa na polisi jamii kuliko kuwa na Sungusungu, Sungusungu hawa hawa watapewa mafunzo watakuwa polisi jamii, haya mambo ya kutoza hela na kunyang’anya simu yatkuwa ndio mwisho wake, na wale wote waliotozwa fedha kinyume cha sharia watarudishiwa fedha zao,” Alisema
Aidha, Mh. Misungwi amewataka wananchi kushiriki vyema katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea na kuhakikisha wanawachagua viongozi bora wachapakazi na sio bora viongozi huku akiwaondoa hofu wananchi wanaodhani kuwa Sungusungu waliofanya uhalifu huo kuwa wametumwa na serikali na kuwahakikishia kuwa serikali ya Dkt. John Pombe Magufuli ipo kwaajili ya kutetea wanyonge na sio kinyume chake.
Maagizo hayo ameyatoa baada ya kusikiliza vilio kadhaa vya wananchi wa Kijiji cha Mfinga na Msila katika kata ya Mfinga Wilayani humo, baada ya wanakijiji hao kupatwa na sintofahamu baada ya kundi la Sungusungu kuvamia vijiji hivyo na kupora fedha za wanakijiji hao na kupelekea taharuki kusambaa hali iliyowakatisha wananchi kushiriki katika kampeni za uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 28.10.2020.
Mmoja wa wanakijiji cha Msila Mashaka Lupondeja alisema kuwa SunguSungu hao walikuwa wanawalazimisha watu kutoa fedha bila ya utaratibu wowote huku wakiwatishia kwa majambia, jambo ambalo liliwakatisha tamaa wakidhani kuwa serikali haipo upande wao na kuwa serikali ndio imewatuma wanyang’anyi hao.
“Unabanwa kabisa msituni, kuna watu hapa wameficha hawajaongea vizuri, milioni tano, milioni 13, milioni 20, milioni 30, hawaongei hapa, wanachomoa jambia moja, mbili anajikamata vizuri anakwambia unatoa au hautoi, kwenye kamsitu wamebana, waue,na wanasema na Magufuli anajua, mimi kipalata kipo nilikuwa sichagui, Magufuli anafaa ila nilikuwa sichagui,” Alisisitiza.
Nae Amour Mohamed wa Kijiji cha Mfinga alisema, “Mtendaji wa kata ndio anajua lile kundi lililopiga watu hapa, na sio leo tu huu ni mwaka wa tatu sungusungu wamechukua hatamu hapa kata hii, viongozi wapo hawataki kuchukua hatua, mwananchi anatozwa mpaka milioni sita, anaambiwa usipolipa tunakuua na watu wanakufa, mi nashangaa uongozi wa Kijiji na wa kata kigugumizi gani wanapata, uwaulize mbele ya mkutano huu”.
Halikadhalika mmoja wa wanakijiji walioporwa fedha na Sungusungu hao Peter Jikuba alisema, “Mh. Mkuu wa Wilaya nilikuwa naomba kwa watu amabao wametozwa mafaini haya, kuna watu walikuwa wanafata haki zao waliotozwa na huyu mtemi aliyetoka hapa, walikuwa wametengeneza operesheni tokomeza majangili, wanakukuta usiku, wanakukamata, wanakutishia visu, wanakutoza faini usiku na kupewa onyo la kwamba usije ukaongea, kwahiyo hao waliokuja kwenye mkutano kusaka haki zao wametozwa tena”.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kijiji cha Msila wakati akielezea tukio la Sungu Sungu hao kukusanya wakazi wa Kijiji hicho uwanjani na kuwapora fedha alisema kuwa, uongozi wa Sungusungu uliofanya hivyo umetoka ngazi ya Tarafa kuja kwenye Kijiji hicho na kubainisha kuwa kulitokea na kutoelewana baina ya uongozi wa Sungusungu wa Kijiji na Tarafa hatimae wananchi wote kuhusishwa katika sakata hilo kwa kukusanywa uwanjani.
“Kwasababu jana yae ile kamati mpya ilikuwa imekabidhiwa fedha kutoka kwenye ile kamati ya zamani, baada ya kukabidhiwa fedha ile kamati mpya kumbe hatunzi mtu mmoja, huwa wanagawana, alianza kusomwa mmoja baada ya mwingine, wewe kwako ziko ngapi, laki tatu weka hapa, wewe, laki mbili, weka hapa, wakarejesha fedha zote lakini baada ya hapo zilifuata adhabu,” Alisimulia.
Post a Comment