Ads

Wananchi wausiwa kutunza amani wakati wa kampeni za uchaguzi na sio kuvunja udugu

Wananchi Mkoani Rukwa wameusiwa kuendelea kuitunza amani katika kipindi chote cha kampeni wakati tukielekea kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika siku ya Jumatano tarehe 28.10.2020 utakaowapa nafasi ya kuwachagua Madiwani katika ngazi za Kata, Wabunge katika ngazi za Majimbo pamoja na kumchagua Rais wa nchi ya Tanzania.

Usia huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alipotembelea baadhi ya vijiji wilayani Nkasi ili kuhamasisha utulivu na kuasa wananchi kutovunja udugu kwasababu za kisiasa hali itakayowapelekea kushindwa kushirikiana na kufanya maendeleo katika vijiji vyao hasa baada ya kuisha kwa uchaguzi huo na washindi kupatikana.

Aidha amewataka wanaoshiriki katika kampeni hizo kutotumia lugha za matusi na kutanguliza kuheshimiana bila ya kusahau kuwa kinachowaunganisha ni udugu uliopo baina yao na hivyo wasijisahau wakatawaliwa na maneno yasiyo na ustaarabu na zaidi kutokubali kuvurugwa na kauli za wanaojinadi na wanaohamasisha vurugu katika kampeni zao.

“Niwaombe ndugu zangu wakati wa kampeni, sisi sote ni ndugu, huyu anaweza akawa yupo CHADEMA, huyu NCCR – Mageuzi, yule wa Chama cha Mapinduzi, lakini sisi sote si ndugu, kwanini mpigane ngumi kwasababu ya uchaguzi, kwanini mtoane ngeu wakati wa uchaguzi, uchaguzi unakwisha, mwezi Novemba raisi anasimikwa pale anaapishwa, ninyi si tutaendelea kuwa ndugu? Sasa kwanini muuane kwasababu hiyo?” Alihoji.

“Watu wakija na kampeni zao wakifanya mbwembwe, wakihamasisha kupigana, mkatae mambo ya fujo kwasababu ninyi mnaishi pamoja ni ndugu, hayo mambo yatapita mpaka tena baada ya miaka mitano, kwahiyo mimi natahadharisha kwamba kipindi cha kampeni, kampeni zifanyike za kistaarabu, lakini watu waheshimiane, kusiwe matusi tukijua kwamba sisi ni ndugu,”Alisema.

Kampeni za Uchaguzi wa Mwaka huu zinatarajiwa kuanza tarehe 26.8.2020 huku wabunge mbalimbali wakiendelea kuchukua na kurudisha fomu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutoka kwa wasimamizi wa majimbo katika halmashauri mbalimbali, halikadhalika wagombea Urais 17 wa vyama 17 nchini wamejitokeza kuwania kiti hicho ambacho Mh.Dkt. John Pombe Magufuli anakiwania kwa muhula wa pili.

Maelezo ya Picha

Mkuu wa mkoa wa Rukwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Miangalua, kata ya Kate Wilayani Nkasi wakati alipotembelea baadhi ya vijiji kuhamasisha utulivu wakati wa kampeni za uchaguzi 2020.

No comments