Wananchi lukuki wamenufaika na ushirika - Waziri Hasunga
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Simiyu
Serikali Imesema kuwa Vyama vya Ushirika vimekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma bora na kuleta ustawi wa Maendeleo ya Taifa letu ambapo Wanachama wa Vyama vya Ushirika wamepata manufaa mbalimbali ya kuwemo kwenye ushirika, ikiwa ni pamoja na bei nzuri ya mazao yao.
Kipato kilichopatikana kimewawezesha kununua vyombo vya usafiri, kujenga nyumba bora na kuwasomesha watoto wao katika ngazi mbalimbali za elimu na wengine wamefikia hadi elimu ya Chuo Kikuu na wengine wameweza kugharimia matibabu ya familia zao.
Waziri Kilimo Japhet Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 3 Agosti 2020 wakati akielezea kuhusu mchango wa sekta ya Ushirika katika uchumi na uzinduzi wa mifumo na kutambua michango ya wadau katika siku ya kuhamasisha Ushirika Kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya wakulima (Nanenane).
Amesema kuwa Vyama vya ushirika wa Akiba na Mikopo vimeendelea kutoa huduma za kifedha kwa wanachama wake ambapo thamani ya mikopo iliyotolewa imeongezeka kutoka Shilingi trilioni 1.3 Desemba, 2018 na kufikia Shilingi trilioni 1.5 Desemba, 2019 sawa na ongezeko la asilimia 15.
Vilevile, amesema kuwa jumla ya thamani ya hisa, akiba na amana imeongezeka kutoka Shilingi bilioni 654 Desemba, 2018 na kufikia Shilingi bilioni 819 Desemba, 2019 sawa na ongezeko la asilimia 25.
Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kuuza mazao yao kupitia vyama vya ushirika ili kuwawezesha kunufaika na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala.
Naye mgeni rasmi katika sherehe hizo Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa uamuzi wake madhubuti wa kuvifuta vyama vya ushirika 2,539 ambavyo vilikuwa na utendaji mbovu uliosababisha kero kwa wanaushirika nchini.
Amesema hatua hiyo ya wizara itawezesha wanaushirika ambapo ni wakulima, wavuvi na wafugaji kunufaika na kazi zao ndani ya ushirika .
“Ninawapongeza sana Wizara kwa hatua mliyochukua ya kuvifuta vyama vya ushirika 2,539 kwa sababu ya kutofanya kazi iliyokusudiwa.” alisema Waziri Kairuki.
Waziri Kairuki alisema katika kipindi cha 2018/2019 jumla ya viwanda 75 vimeanzishwa na vyama vya ushirika vinavyochata alizeti, chikichi,kutengeneza samani za majumbani,kuchakata pamba na mazao ya nafaka pamoja na usindikaji wa maziwa.
“ Viwanda vinavyomilikiwa na vyama vya ushirika vimeongezeka kutoka viwanda 133 mwaka 2018 hadi kufikia viwanda 208 mwaka 2019” alisema Waziri Kairuki.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ameiagiza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (EGA) kuangalia namna bora ya kuweka mfumo shirikishi wa TEHAMA utakaoweza kuongeza uwazi katika usimamizi wa vyama vya ushirika hususan AMCOS.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga amesema katika kipindi hicho, mazao ya ufuta, kakao, maziwa, pamba, chai, tumbaku, korosho, zabibu, kahawa na mazao mchanganyiko yenye thamani ya Shilingi trilioni 2.9 yaliuzwa kupitia ushirika kwa aidha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala na au mkataba.
"Mifumo hii imewasaidia wakulima na wanunuzi kupata mazao yenye ubora kwa kuzingatia madaraja, bei ya ushindani na masoko ya uhakika kwa mazao yao" Amekaririwa Waziri Hasunga
Amesisitiza kuwa Sekta ya Ushirika imekuwa na mchango mkubwa katika kutoa ajira kwa wananchi nchini ambapo hadi kufikia Desemba 2019, zaidi ya wananchi 90,090 wamepata ajira zikiwemo ajira za kudumu, mkataba na za msimu ikilinganishwa na ajira 32,668 Desemba, 2018.
"Kauli mbiu katika maonesho ya mwaka huu inasema “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua Viongozi Bora 2020. Wakulima, wafugaji na wavuvi wa nchi hii wapo tayari kwa Uchaguzi na kupitia kwako wanatoa salamu zao kuwa kwa mafanikio ambayo serikali ya Awamu ya Tano imepata katika sekta hizi, watakipatia Chama cha Mapinduzi ushindi mnono" Amesisitiza Waziri Hasung
Aidha, amewaomba Wanaushirika kuchagua viongozi bora katika vyama vyao kwakuwa viongozi ndio chachu ya maendeleo ya Vyama hivyo.
Post a Comment