Ads

Serikali Yavunja Rekodi Ukuaji wa Uchumi

Mwambawahabari

.......................................................

Na. Immaculate Makilika na Frank Mvungi- MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kuvunja rekodi ya ukuaji wa uchumi wa nchi katika kipindi cha miaka minne ya utawala wake sambamba na kupunguza mfumuko wa bei kutoka wastani wa asilimia 9.2 mwaka 2015 hadi asilimia 4.3 mwaka 2019/2020.

Akizungumza katika Mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni semaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi alisema sasa pato la Taifa (GDP) ni kubwa kuliko miaka yote tangu uhuru na kufanya uchumi wa Tanzania kuwa wa 10 barani Afrika na mfumuko wa bei kuwa mdogo kuliko wakati wowote katika historia ya Tanzania.

“Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano, pato la Taifa limekua kwa wastani wa shilingi trilioni 124 kwa mwaka ikilinganishwa na wastani wa shilingi trilioni 52.9 kwa mwaka katika kipindi cha Awamu ya Nne” alieleza Dkt. Abbasi.

Aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli imesimamia na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa ukuaji mzuri wa uchumi. Aidha, katika miaka minne (2016-2019) uchumi wa Tanzania umekuwa kwa wastani wa asilimia 6.9 kwa mwaka, wastani ambao ni mkubwa ikilinganishwa na Awamu zote.

Dkt. Abbasi alisema kuwa msingi mwingine muhimu katika ukuaji wa uchumi wa nchi na katika kutekeleza azma ya kujitegemea umekuwa ni kuongeza mapato ya Serikali kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 mwaka 2015 hadi shilingi trilioni 1.3 mwaka 2016, 2018/19 na Julai, 2019 hadi Juni, 2020 umefikia wastani mpya wa shilingi trilioni 1.5 (ambapo kwa mwezi Disemba, 2019 na Juni 2020   imekusanywa trilioni 1.9 mtawalia).

Serikali ya Awamu ya Tano, imefanikiwakuongeza mapato yasiyo ya kodi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 688.7 mwaka 2014/2015 hadi kufikia shilingi trilioni 2.4 mwaka 2018/2019. Ambao kuongezeka kwa mapato hayo mapato yasiyo ya kodi ni matokeo ya kubana mianya ya kukwepa kodi, muamko wa wananchi kulipa kodi, usimamizi mzuri wa Wizara ya Fedha, TRA na Serikali kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Dkt. Abbasi alisem kuwa Taasisi za kimataifa zimeendelea kusifia ukuji wa uchumi wa nchi ambapo Septemba 30, 2019 Benki ya Dunia iliitaja Tanzania kuwa ni nchi yenye uchumi unaokuwa kwa wastani wa  asilimia 6 hadi 7 kwa mwaka katika kipindi cha miaka 10.

“Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeitaja Tanzania kuwa nchi yenye uchumi jumuishi wenye kuzingatia maslahi ya umma, uwekezaji imara na unaokuwa pamoja na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa za nje. Aidha, Machi, 2020 Shirika la Fedha Duniani limesema hali ya uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara ukikua kwa zaidi ya asilimia 6, mfumuko wa bei ukiwa chini ya asilimia 5 na akiba ya fedha za kigeni ikiwa ya kutosheleza na deni la taifa likiwa himilivu.” Alisema Dkt. Abbasi

Halikadhalika jarida la Forbes linaitaja Tanzania kuwa nchi ambayo uchumi wake umekua kwa wastani wa aslimia 6 hadi asilimia 7 kwa mwaka kutokana  na matumizi mazuri ya rasilimali zake na utalii kati ya mwaka 2009 hadi 2017.

Fauku ya hayo, Dkt. Abbasi alisema kuwa miaka mitano ijayo Serikali itaendelea kuweka sera, mipango na mikakati, kusimamia na kulinda misingi ya uchumi na nchi kuendelea kuwa katika uchumi wa kati.

Aidha, Msemaji Mkuu wa Serikali amewataka watanzania kushiriki katika maendeleo ya uchumi  kwa kufanyakazi kwa bidii, kuepuka rushwa na  uvivu kazini, kulipa kodi na kushiriki kutumia fursa zinazojitokeza  katika ukuaji wa uchumi na kutoa maoni kwa Serikali katika kuboresha uchumi wa nchi.
Mwisho

No comments