MKUCHIKA AITAKA TAKUKURU KUHAKIKISHA WANANCHI WANAPATA HAKI PINDI WANAPOENDA KUPATA HUDUMA.
Na. James K. Mwanamyoto — Namtumbo
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imetakiwa kuhakikisha wananchi wanapata haki wanazostahili popote pale wanapoenda kupata huduma nchini, iwe ni kwenye taasisi za umma au binafsi.
Agizo hilo limetolewa wilayani Namtumbo jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapt. (Mst) Mhe. George H. Mkuchika wakati akizindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, TAKUKURU inatakiwa kuwajengea wananchi imani ya kiutendaji ili pale inapotokea wananyanganywa haki zao na mtu au taasisi yoyote kwa njia za rushwa, TAKUKURU ndio iwe ni kimbilio lao huku wakiwa na imani kuwa watasaidiwa ipasavyo na taasisi hiyo.
“Nawasihi, endeleeni kuwangata wala rushwa na mafisadi wote ili mradi msimuonee au kumpendelea yeyote, na endeleeni kuifanya haki ndio nguzo ya utendaji kazi wenu wa kila siku,” Mhe. Mkuchika alihimiza.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Bibi Sabina Seja akitoa maelezo kuhusu jengo hilo alisema, uzinduzi wa jengo la TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo ni ushaidi tosha kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli imeonesha nia na dhamira ya dhati ya kukabiliana na vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali za umma nchini.
Bibi Seja, amemtibitishia Mhe. Mkuchika kuwa, Watumishi wa TAKUKURU wilayani Namtumbo watatumia jengo la ofisi hiyo kuhakikisha wanapambana na vitendo vya rushwa, ufisadi na ubadhirifu kwa manufaa ya wananchi na maslahi ya taifa.
Mhe. Mkuchika amezindua jengo hilo la TAKUKURU Wilaya ya Namtumbo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye tangu aingie madarakani amefanya kazi kubwa ya kuimarisha na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini.
Post a Comment