Ads

MAZIWA YA MAMA MIEZI SITA YA MWANZO HUIMARISHA KINGA YA MWILI KWA MTOTO.

Mwambawahabari


Na Maria Kaira,Mwambawahabari 
 Jamii imetakiwa kuelewa kuwa, kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama kwa miezi sita ya mwanzo bila kumpa chakula kingine ,huimarisha kinga ya mwili na akili inayomkinga Mtoto dhidi ya maradhi mengine.

 Hayo yameelezwa  na Mkurugenzi wa Elimu na Mafunzo ya Lishe (TFNC) Sikitu Simon Kihinga Wakati wa ufungua wa semina ya Waandishi wa habari iliyohusu Maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Duniani mwaka 2020 ambayo hufanyika kila Agosti 1-7 ya kila mwaka.

 Bi.Sikitu ameeleza kuwa, mama baada ya kujifungua, anatakiwa kumnyonyesha mtoto, kwa kipandi cha miezi sita ya mwanzo bila kumpa chakula kingine chochote, jambo ambalo litajenga afya ya mtoto, ikiwa ni pamoja na kumjengea kinga ya mwili dhidi ya maradhi ili aweze kukua kimwili na kiakili .

 Amesema maziwa ya mama ni chakula bora kwa mtoto humpatia virutubishi vyote na maji anayohitaji kwa ukuaji katika miezi sita ya mwanzo, pia humsaidia mtoto kukua vizuri pamoja na kuhimarisha kinga dhidi ya magonjwa.

 Pia amesema wiki ya unyonyeshaji wa mwaka huu inaeleza uhusiano uliopo kati ya unyonyeshaji watoto maziwa ya mama na afya bora pamoja na kulinda mazingira ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo inasema” Tuwawezesha wanawake kunyonyesha watoto kwa afya bora na ulinzi wa mazingira”. 

 Maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji wa maziwa ya mama ni fursa muhimu ya kutoa hamasa kwa jamii katika kulinda, kuimarisha na kuendeleza unyonyeshaji ambao umekua suluhisho ambalo linampa kila mtu msingi imara wa mwanzo wa maisha na husaidia kuboresha afya na ustawi wa wanawake na watoto duniani kote.

Afisa Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) Gelagister Gwarasa, amewataka akina Mama kuanza kumnyonyesha mtoto maziwa ya mama katika saa moja ya kwanza mara baada ya kujifungua,Pia kuwa na utaratibu wa kunyonyesha mtoto mara kwa mara ili kuongeza utokaji wa maziwa na kusaidia kupata maziwa yenye maji mengi ambayo hukata kiu ya mtoto.

 Bi.Gelagister amezitaja faida za mama kunyonyesha ikiwemo kusaidia tumbo la uzazi kurudi katika hali ya kawaida na kuzuia uwezekano wa upungufu wa damu kwa mama.

 Madhara ambayo yanaweza kumpata mtoto anayepewa vyakula vingine tofauti na maziwa ya mama akiwa na umri chini ya miezi sita ni pamoja na Utapiamlo, Kupata Mzio (Allergy), Magonjwa ya kuhara, Kupunguza uhusiano kati yake na mama na kupata uzito uliozidi,” Amesema

No comments