MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE ZANZIBAR
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mamboya Kushoto akimkaribisha Balozi Seif kwenye Uwanja wa Ndege wa Kigunda Nungwi kuangalia maendeleo ya ujenzi wa Uwanja huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake akitembelea na kukagua maaendeleo ya Ujezni wa Uwanja wa Ndege wa Kigunda Nungwi Mkoa Kaskazini Unguja.
Muonekano wa njia ya kurukia Ndege kwenye uwanja wa ndege wa Kigunda ambayo iko katika hatua ya uwekwaji wa Kifusi hatua ya mwisho.
Msimamizi wa Ujenzi wa Uwanja wa Kigunda Nungwi Mhandisi George aliyeshika kisemeo akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi juu ya hatua iliyofikiwa ya Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigunda.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege vya Zanzibar Nd. Said Iddi Ndombogani aliyeshika kisemeo akimuhakikishia Balozi Seif kwamba Uwanja huo utakapomalizika utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege kubwa za abiria zikiwemo Foka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiuagiza Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuzingatia upatikanaji wa maeneo ya Ardhi mapema kwa mahitaji yao kabla ya kuvamiwa.
Picha na – OMPR – ZNZ.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameuagiza Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar kuangalia mpango maalum wa muda mrefu utakaozingatia mahitaji halisi ya maeneo ya kazi kwa ajili ya Miradi yao ya Maendeleo.
Alisema Mpango huo endapo utazingatiwa katika hatua za awali mbali ya kusaidia kupunguza gharama za fidia kwa mali za Wananchi lakini pia utatoa fursa kubwa zaidi kwa Mamlaka hiyo kujipangia Mipango yao kwa mujibu wa Muongozo na vigezo vya Kimataifa vinavyopaswa kutekelezwa katika jukumu lao ya kila siku.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa agizo hilo wakati alipofanya ziara fupi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kigunda uliopo pembezoni mwa Mji wa Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja ambao kwa sasa ndege ndogo ndogo zinauwezo wa kuruka na kutua.
Alisema yapo matukio kadhaa yanayoendelea kushuhudiwa katika Jamii ambapo Serikali hulazimika kulipa fidia kutokana na miradi mbali mbali inayotekelezwa na Taasisi za Umma baada ya maeneo yanayoanzishwa miradi hiyo kuwa na Mali za Wananchi.
Balozi Seif aliutaka Uongozi wa Mamlaka hiyo ya Viwanja vya Ndege Zanzibar kuhakikisha kwamba kazi hiyo wanaitekeleza katika kipindi hichi kabla ya baadhi ya Watu kuanza kuvamia maeneo hayo baada ya kuanza kwa harakati za Uwanja huo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya ndege Zanzibar kwa jitihada zao za kusimamia ujenzi wa Uwanja huo wa Ndege wa Kigunda na kuushauri katika harakati zao ni vyema zikaenda sambamba na kujengewa uzio utakaoepusha uingiaji wa kiholela kwenye eneo hilo.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeridhia kujengwa kwa Uwanja huo kutokana na mabadiliko makubwa ya mwenendo mzima wa shughuli za Utalii, Biashara pamoja na Mawasiliano ya usafiri wa anga kati ya Zanzibar, Mikoa ya Tanzania Bara na hata Nchi jirani.
Balozi Seif alibainisha kwamba Watalii waliojipangia kufanya matembezi katika Ukanda wa Kaskazini mwa Kisiwa cha Unguja kutokana na uwepo wa Uwanja huo wanaweza kwenda moja kwa moja kwa kutumia ndege kutoka maeneo tofauti badala ya usafiri wa Gari ambao kwa sasa umezidi msongamano mkubwa.
“ Kwa vile Uwanja huo utakapomalizika utakuwa na uwezo wa kuhudumia ndege zitakazobeba Abiria Zaidi ya 70 utasaidia kupunguza pia msongamano katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kufikiria wazo jengine la kuangalia uwezekano wa kuwepo kwa Kiwanja chengine cha Ndege katika Ukanda wa Kusini mwa Kisiwa cha Unguja kwa lengo la kuimarisha huduma za Kiuchumi Nchini.
Mapema Msimamizi wa Ujenzi wa Uwanja huo wa Ndege wa Kigunda Nungwi Mhandisi George alisema kazi zinazoendelea Uwanjani hapo kwa sasa ni ukamilishaji wa Uwekaji wa Kifusi kwa tabaka la Mwisho.
Mhandisi George alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hatua ya utandikaji wa Lami kwenye Uwanja huo inatarajiwa kuanza Mwezi wa Oktoba Mwaka huu ukiwa na urefu wa Kilomita Mbili zitakazowezesha kutua au kuruka kwa ndege tofauti kubwa zikiwemo Foka.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar Nd. Said Iddi Ndombogani alisema Ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kigunda ni moja miongoni mwa Miradi mikubwa inayotekelezwa na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Usafiriashaji Zanzibar ndani ya Mpango Kazi wake.
Nd. Ndombogani alisema mradi huo utahitaji kuwa na eneo lenye ukubwa wa Hekta 400 zitakazofanana na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro ambao utawezesha ndege kubwa za aina yoyote kuweza kuruka au kutua bila ya mashaka.
Alisema huduma zote zitakazohitaji kwa mujibu wa vigezo vya Kimataifa zinatarajiwa kupatikana kwenye Uwanja huo pale utakapomalizika kabisa sambamba na Nyumba za Wafanyakazi watakaotoa huduma katika Uwanja huo.
Matayarisho ya ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Kigunda Nungwi zilianza rasmi mwishoni mwa Mwaka 2019 ambapo jiwe la msingi la kuanza ujenzi huo liliwekwa na Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Mgezni Juma Hassan mnamo Tarehe 10 Januari 2020 ndani ya shamra shamra za sherehe za Mapinduzi Matuku ya Mwaka 1964 kutimia Miaka 56.
Post a Comment