Ads

TASAC MUDA MCHACHE MAFANIKIO LUKUKI

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema kuwa kwa mwaka huu linatarajia kutoa gawio kwa Serikali la zaidi ya Sh. Bilioni 20.

Aidha TASAC imetangaza nafasi 60 za ajira katika shirika hilo hivyo limewaomba vijana kujitokeza kwa wingi kuomba nafasi hizo ili waweze kufanya kazi na kuinua uchumi wa nchi.

Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Emmanuel Ndomba wakati akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya maonesho ya 44 ya biashara ya kimataifa yanayoendelea jijini Dar es Salaam. 

Ndomba amesema wamekuwa wakifanya majukumu mbalimbali yakiwamo ya uhakiki wa mizigo, uangaliaji na uhakiki wa nyaraka zote za mizigo inayokuja Tanzania kwa njia ya meli, na kuongeza kuwa kazi hizo ndizo zimekuwa zikiwangizia fedha zinazowawezesha kulipana mishahara na kutoa gawio kwa Serikali.

"Mwaka jana tuliweza kutoa gawio kwa Serikali kiasi cha Sh. Bilioni 10, na mwaka huu tunatarajia kuchangia mara mbili zaidi ya tulivyofanya mwaka jana, pia tumefanikiwa kutengeneza ajira kwani tumeshatangaza ajira 60 kwa vijana ambao wakipatikana watafanya kazi katika sekta zote tulizonazo," amesema

Amesema kwenye uchumi endelevu lazima kipengele cha usajili na kuongeza kuwa asilimia 90 ya mizigo yote inayosafirishwa duniani inapitia baharini.

"Tanzania tuna habati kwani tunaeneo kubwa la bahari na Serikali ilifanya vema kuwa na chombo hiki cha TASAC ambacho kinahakikisha kwamba ufanyaji wa biashara katika meli unalinda pia mazingira na usalama yanalindwa, jambo hilo tumelifanya kwa juhudi kwani tumekuwa tukitoa elimu kwa watumiaji na wasafiri kuhusu nini wafanye wanapokuwa katika vyombo hivyo baharini," amesema

Kuhusu ajira, amesema ajira walizozitangaza ni kwa wale vijana wenye ujuzi, uzoefu na utaalamu wa kuondoa mizigo na bidhaa  na kuongeza kuwa watakaopatikana watasambazwa katika sehemu zote wanazozifanyia kazi ambazo ni mipaka, viwanja vya ndege na bandarini.

No comments